1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makundi ya waasi yaondoka Ghouta Mashariki

Isaac Gamba
27 Machi 2018

Watu wapatao 7,000 wameondoka Ghouta Mashariki leo Jumanne kuelekea  jimbo linalodhibitiwa na waasi kaskazini mwa Syria chini ya makubaliano yaliyoandaliwa na Urusi yanayolenga  kulikabidhi eneo hilo kwa serikali.

Syrien Reisebus-Konvoi Evakuierung aus Ost-Ghouta
Picha: Getty Images/AFP/A. Eassa

Kwa mujibu wa shirika la waangalizi wa haki za binadamu nchini Syria msafara wa karibu mabasi 100 miongoni mwao wakiwemo wapiganaji wa makundi ya waasi, familia zao pamoja na raia wengine umeondoka mapema leo asubuhi kutoka  eneo linalodhibitiwa na kundi la upinzani la  Faylaq al-Rahman,  kuelekea  kaskazini mwa Syria.

Hatua hiyo ni sehemu ya makubaliano  yaliyofikiwa wiki iliyopita kati ya kundi hilo la itikadi kali  na  Urusi ambayo inaisaidia  Syria kujadili makubaliano hayo yanayolenga kuliondoa kundi la mwisho la waasi katika eneo la Ghouta Mashariki.

Majeshi ya Urusi yanayowaunga mkono wapiganaji wa serikali ya Syria pamoja na wanamgambo washirika wamekuwa wakifanya mashambulizi makali tangu Februari 18 ambapo wamefanikiwa kukomboa zaidi ya asilimia 90 ya eneohilo lililo jirani  na mji mkuu Damascus.

Makubaliano na kundi la itikadi kali la Faylaq al-Rahman yalitangazwa Ijumaa iliyopita na utekelezaji wake ulianza siku iliyofuata.  Kiasi ya watu 1,000 wakiwemo waasi, ndugu zao na raia wengine waliondolewa Jumamosi iliyopita na kufuatiwa Jumapili iliyopita  na kundi lingine la watu 5,435.

Rais wa Syria  Bashar Assad amekuwa akitumia makubaliano ya aina hiyo kukomboa maeneo yaliyokuwa yanadhibitiwa tangu vuguvugu dhidi ya serikali yake lilipoanza miaka saba iliyopita.

Hatua hiyo ni mafanikio kwa Assad

Rais wa Syria Bashar AssadPicha: Reuters

Kukombolewa moja kwa moja kwa Ghouta Mashariki itakuwa ni ushindi mkubwa kwa Assad tangu Desemba 2016 wakati vikosi vyake  kwa msaada wa  Urusi vilipofanikiwa kukomboa mji wa Aleppo uliokuwa ukidhibitiwa na makundi ya upinzani.

Wakati hayo yakiendelea Jeshi la Uturuki usiku wa kuamkia leo limewaua wanamgambo 11 wa Kikurdi katika jimbo  la Hatay linalopakana  na Syria hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa Gavana wa jimbo hilo. Taarifa za kijeshi zimesema  wanajeshi wawili wameuawa katika shambulizi lililofanyika kwenye mkoa wa Afrin nchini Syria.

  Kwa msaada wa mashambulizi ya anga, vikosi vya usalama vya Uturuki vilifyatua risasi na kuwaua wanamgambo baada ya kuwaona katika wilaya ya Hatay  jirani na bahari ya Mediterranea.  Hiyo ni kwa mujibu wa taarifa ya serikali ya Uturuki.

 Tangu mwaka 1984 Uturuki imekuwa ikipambana na wanamgambo wa kikurdi wa chama cha wafanyakazi cha PKK kilichopigwa marufuku nchini humo na zaidi ya watu 40,000 wameuawa katika mapigano ambayo yamejikita kwa kiwango kikubwa kusini mashariki mwa Uturuki  kilomita kadhaa mashariki mwa mji wa Hatay.

Januari mwaka huu jeshi la Uturuki pamoja na washirika wake waasi wa Syria  lilianzisha mashamulizi dhidi ya wapiganaji wa kikurdi wa YPG katika mji wa Afrin nchini Syria  unaopakana na Hatay na mwishoni mwa wiki kufanikiwa kudhibiti kwa kiwango kikubwa mji huo.

Uturuki inawachukulia wapiganaji wa YPG kama  magaidi na muendelezo wa chama cha PKK kilichopigwa marufuku  lakini kwa upande mwingine wapiganaji wa YPG ni washirika wa Marekani katika mapambano dhidi ya kundi la itikadi kali linalojiita Dola la Kiisilamu nchini Syria.

Mwandishi: Isaac Gamba/rtre/ape

Mhariri    : Gakuba, Daniel

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW