1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makundi ya jihadi yazusha wasiwasi Afrika Magharibi

18 Novemba 2022

Nchi za pwani ya Afrika Magharibi zimefanya mazungumzo kuhusu kuimarisha ushirikiano kuyakabili machafuko yanayoongezeka yanayofanywa na makundi ya jihadi kutoka ukanda wa Sahel.

Mali | Soldat mit Ak-47
Picha: KENZO TRIBOUILLARD/AFP/Getty Images

Benin,Ghana,Ivory Coast na Togo nchi ambazo ni jirani ya ghuba ya Guinea  zinazidi kukabiliwa na kitisho kinachoongezeka kutoka makundi ya itikadi kali ya wanamgambo wa  Dola la Kiiislamu na Alqaeda ambayo yanaendeleza vita katika maeneo ya mipaka ya nchi hizo ya kaskazini mwa ukanda wa Sahel.

 Na mkutano uliofanyika jana alhamisi baina ya viongozi wa nchi hizo umejikita katika kuangalia ni kwa namna gani zinaweza kushirikiana kukabiliana na kitisho hicho baada ya nchi zaidi kutangaza zitaondowa wanajeshi wao katika ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Mali.

Picha: Leon Neal/Getty Images

Kama sehemu ya kile kinachojulikana kama juhudi za Accra,wawakilishi kutoka nchi hizo za pwani ,Umoja wa Ulaya na wadau wengine walikutana katika mji mkuu wa Ghana,Accra kwa ajili ya mazungumzo kuhusu  usalama na ushirikiano wa kiintelijensia.

Mapendekezo

Waziri wa usalama wa Ghana Albert Kan Dapaah alisema ushirikiano unahitajika kutokana na kitisho cha makundi ya itikadi kali ambacho kimeongeza- na kusambaa  kuliko ilivyofikiriwa awali na kinavuka mipaka.

Akitowa ufafanuzi zaidi kuhusu ukubwa wa kitisho hicho alisema katika robo ya kwanza ya mwaka huu 2022, bara la Afrika limeshuhudia mashambulizi mara 346 ambayo takriban nusu yalifanyika magharibi mwa bara hilo. Juhudi za Accra ni mpango ulioanzishwa mwaka 2017- ukizijumuisha Benin,Togo,Ghana,Ivory Coast pamoja na Burkina Faso,wakati Mali na Niger nazo pia zilijiunga.

Mkutano huo ulioanza jana utakwenda mpaka wiki ijayo na pia utawajumuisha wawakilishi kutoka Umoja wa Ulaya nc serikali ya Uingereza pamoja na wanachama 15 wa jumuiya ya kiuchumi ya nchi za magharibi mwa Afrika ECOWAS.Aidha mkutano wa kilele wa kikanda utakaowaleta pamoja viongozi wakuu wa nchi umepangwa kufanyika wiki ijayo tarehe 22 ambapo viongozi hao watajadili kuhusu mapendekezo ya kiusalama.

Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Mgogoro unaosababishwa na makundi ya itikadi kali katika kanda ya Sahel ulianzia kaskazini mwa Mali mnamo mwaka 2012 na kusambaa mpaka BurkinaFaso na Niger mnamo mwaka 2015 na hivi sasa nchi zilizoko katika ghuba ya Guinea zinapata tabu kwa kuandamwa na mashambulizo ya mara kwa mara ya magaidi.

Katika nchi hizo maelfu ya watu wameuwawa na zaidi ya milioni mbili wameachwa bila makaazi na uharibifu mkubwa umeshuhudiwa katika nchi hizo tatu masikini kabisa duniani.

Ufaransa na nchi nyingine kadhaa katika ujumbe wa kulinda amani zimekuwa zikiendesha harakati za kijeshi nchini Mali kwa takriban muongo mmoja kuzuia kusambaa kwa machafuko yanayosababisha makundi hayo ya itikadi kali.

Lakini baada ya kushuhudiwa mapinduzi ya kijeshi mara mbili nchini Mali,utawala wa huo wa kijeshi ulijisogeza zaidi upande wa kambi ya Urusi na kupokea silaha na kuruhusu kile kinachoitwa na nchi za magharibi  mamluki wa Urusi,kuendesha operesheni za kijeshi.Hatua hiyo bila shaka imeyaharibu kabisa mahusiano na washirika hao wa nchi za Magharibi.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW