1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Makundi yenye silaha Myanmar yadhibiti kivuko cha mpakani

26 Novemba 2023

Muungano wa makundi ya makabila madogo yaliyojihami kwa silaha nchini Myanmar, umedai kudhibiti kivuko muhimu cha mpakani kuelekea China kutoka kwa utawala wa kijeshi nchini humo.

Myanmar | Mzozo
Wapiganaji wa muungano wa makundi ya makabila madogo yaliyojihami kwa silaha nchini Myanmar- MNDAAPicha: Kokang Information Network/AFP

Muungano wa makundi ya makabila madogo yaliyojihami kwa silaha nchini Myanmar, Myanmar National Democratic Alliance Army (MNDAA) limechukuwa udhibiti wa kivuko muhimu cha mpakani kuelekea China kutoka kwa utawala wa kijeshi nchini humo. Haya yameripotiwa leo na vyombo vya habari vya ndani na chanzo kimoja cha usalama.

Soma taarifa inayohusiana: China na Myanmar zasaka amani kufuatia ghasia za mpakani

Shirika la habari la Kokang linalohusishwa na MNDAA, limeripoti leo kuwa kundi hilo limechukuwa udhibiti wa lango la mpakani la Kyin San Kyawt.

Kokang, imeongeza kuwa muungano huo wa makundi ya wapiganaji ambao pia unajumuisha jeshi la Arakan (AA) na jeshi la ukombozi la Ta'ang National (TNLA) umechukuwa udhibiti wa maeneo mengine katika eneo la kibiashara la mpakani baada ya shambulio hilo kuanza siku ya Ijumaa.

Mapigano yameendelea katika jimbo la Shan kaskazini mwa Myanmar, karibu na mpaka wa China, baada ya muungano huo kuanzisha mashambulizi dhidi ya jeshi mwezi Oktoba.