1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makundi yenye silaha yashika doria Tripoli

16 Desemba 2021

Makundi yenye silaha yalishika doria katika mitaa mbalimbali mjini Tripoli usiku wa kuamkia Alhamisi kufuatia hatua ya kufutwa kazi kwa afisa mmoja wa jeshi wa ngazi ya juu. 

Kämpfe in Libyen
Picha: dapd

Afisa mmoja wa jeshi ambaye hakutaka jina lake litambulishwe, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba makundi yenye silaha ambayo yako chini ya vikosi mbalimbali vya kijeshi yalishika doria katika maeneo muhimu mjini Tripoli.

UN yafuatilia majaribio ya kuzuia mchakato wa uchaguzi Libya

Amesema hatua hiyo ilijiri saa chache baada ya Jenerali Abdulkader Mansour kuchukua wadhiwa wake mpya kama kamanda wa jimbo la Tripoli, kufuatia amri ya Baraza la urais ambalo ndilo linaongoza jeshi rasmi la taifa hilo.

Mansour amechukua nafasi ya Abdulbasit Marwan ambaye kwa miaka mingi aliushikilia wadhifa huo unaoungwa mkono na makundi yenye silaha na ambayo yana nguvu nyingi mjini Tripoli.

Picha zilizosambaa usiku wa kuamkia leo kwenye mitandao ya kijamii zilionesha makumi ya watu wenye silaha, waliotizamwa kuwa wafuasi wa Marwan pamoja na magari ya kijeshi nje ya makao makuu ya waziri mkuu wa mpito Abdulhamid Dbeibah, na vilevile nje ya majengo mengine muhimu.

Afisa wa kijeshi aliyezungumza na AFP alipuuza wasiwasi wowote akisema hatua hiyo ilichukuliwa na vikosi vinavyolinda majengo na taasisi za serikali na kwamba hawakuwa wameyazingira maeneo hayo.

Khalifa Haftar, mbabe wa kivita ambaye vikosi vyake vinadhibiti mashariki ya Libya pia ametangaza kuwania urais.Picha: Ayhan Mehmet/AA/picture alliance

Makundi yenye silaha yanayodhibiti Tripoli

Libya imekuwa katika hali ya misukosuko tangu aliyekuwa rais wa nchi hiyo Moammar Gaddafi alipopinduliwa mwaka 2011.

Hadi sasa makundi mbalimbali yenye silaha yanadhibiti mji mkuu Tripoli. Baadhi ya makundi hayo yana mafungamano na wizara ya ulinzi na mambo ya ndani.

Hali hiyo ya kiusalama mjini Tripoli inajiri wakati kuna wasiwasi mwingi ikiwa uchaguzi wau rais ambao umepangwa kufanyika Disemba 24 utafanyika au la.

Uchaguzi huo ni sehemu ya juhudi za jamii ya kimataifa zinazoongozwa na Umoja wa Mataifa, kujaribu kuleta amani na kuiunganisha nchi hiyo iliyogawika kutoka na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa muda wa muongo mmoja uliopita.

Hadi sasa orodha rasmi ya wale watakaogombea urais haijatangazwa  na tume inayosimamia uchaguzi.

Mashaka ya kufanyika uchaguzi Disemba 24

Wakati huo huo, Abu Bakr Marada ambaye ni mwanachama wa tume inayosimamia uchaguzi Libya amekiambia kituo cha televisheni cha Aljazeera leo Alhamisi kwamba, hali imekuwa ngumu kwa uchaguzi kuandaliwa Disemba 24.

Kuna mgawanyiko kuhusu uchaguzi. Upande mmoja unataka ufanyike na upande mwingine unataka uahirishwe. Wakosoaji wanatahadharisha kwamba kuendelea na mipango ya uchaguzi kunaweza kuitumbukiza nchi katika machafuko mapya.

Mwanaye rais wa zamani Moammar Gaddafi- Saif al-Islam Gaddafi ambaye ametangaza kuwania urais Libya.Picha: Mast Irham/dpa/picture alliance

Wanasema Libya ingali imegawika zaidi baina ya pande zenye silaha. Na kuna uwezekano kwamba pande hizo zitayapinga matokeo ikiwa ushindi utaenda kwa wapinzani.

Takriban watu 100 wametangaza kuwania urais. Tume inayosimamia uchaguzi ilitarajiwa kutangaza orodha rasmi ya wagombea wiki iliyopita, lakini haijatoa orodha hiyo rasmi kwa sababu ya mapingamizi ya kisheria.

Mgawanyiko kuhusu baadhi ya wagombea urais

Utata kuhusu uchaguzi huo ulitanda zaidi baada ya Khalifa Haftar ambaye ni mbabe wa kivita ambaye vikosi vyake vinadhibiti mashariki ya Libya kutangaza kuwa atawania urais. Aidha tangazo la mwanaye rais wa zamani Gaddafi- Seif al-Islam kuwa atawania pia iliongeza mtafaruku.

Haftar anayetizamwa kama shujaa upande wa mashariki hapendwi na wengi upande wa magharibi mwa nchi.

Kwa upande wake Seif al-Islam, wapo wanaotizama kuwania kwake kama jaribio la kutaka kuirejesha Libya katika enzi za udikteta.

(AFPE, RTRE)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW