1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Malawi kufanya uchaguzi wa marudio Julai 2

23 Machi 2020

Uchaguzi wa urais nchini Malawi unatarajiwa kurudiwa tena Julai 2, kufuatia amri ya mahakama ya juu nchini humo, baada ya matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika mwaka jana kufutwa kufuatia udanganyifu

Malawai Blantyre | Präsidentenwahl - Jane Ansah Vorsitzende des Wahlgremium gibt Ergebnisse bekannt
Picha: picture-alliance/dpa/XinHua/P. Lijun

Uchaguzi wa urais nchini Malawi unatarajiwa kurudiwa tena Julai 2, kufuatia amri ya mahakama ya juu nchini humo, baada ya matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika mwaka jana kufutwa kufuatia udanganyifu, tume ya uchaguzi nchini humo imesema Jumatatu hii.

"Kufuatia maamuzi ya mahakama ya katiba ya Februari 3, yaliyofuta matokeo ya uchaguzi wa urais na kuagiza kufanyika uchaguzi mpya, kwa sababu ya dosari tunatangaza kwamba chaguzi zitafanyika Julai 2,” mwenyekiti wa tume hiyo Jane Ansah amewaambia mkutano wa waandishi wa habari.

Katika maamuzi ya kwanza kabisa kuwahi kufikiwa nchini humo, mahakama ilibatilisha matokeo ya uchaguzi wa Mei 21, yaliyomrejesha mamlakani kwa awamu ya pili rais Peter Mutharika.

Mahakama ilisema matokeo ya uchaguzi kwa kiasi kikubwa yaligubikwa na udanganyifu na hususan "matumizi makubwa ya wino mweupe wa masahihisho kwenye karatasi za kupigia kura”.

Iliagiza kufanyika kwa chaguzi mpya katika kipindi cha siku 150, lakini Mutharika alikatia rufaa maamuzi hayo. Rufaa yake hiyo itasikiliywa na mahakama ya juu Zaidi kuanzia Aprili 15.

Upinzani ulikwenda mahakamani kupinga matokeoPicha: Getty Images/AFP/A. Gumulira

Rais Mutharika hadi sasa bado hajakubali kusaini mapendekezo kuhusu mabadiliko ya sheria ya uchaguzi yanayotaka mtu kupata wingi wa zaidi za asilimia 50 ili kuingia mamlakani kwa awamu ya pili.

Mapendekezo hayo ni kizingiti kikubwa kwa Mutharika, ambaye alitangazwa mshindi kwa ushindi wa asilimia 35.8 tu ya kura.

Ansah, amesema iwapo rais atagoma kuyaridhia mapendekezo hayo ya sharia mpya kabla ya siku ya uchaguzi, basi tume ya uchaguzi italazimika kuandaa uchaguzi chini ya sheria zilizopo.

Ili kujiwekea mazingira mazuri zaidi kwenye uchaguzi unaokuja, pande kuu mbili zinazopingana wiki iliyopita zilisaini makubaliano baina yao kuelekea kwenye uchaguzi huo.

Chama cha upinzani cha Malawi Congress, MCP pamoja na United Transformation Front, UTM walisaini makubaliano ya kuungana kwenye uchaguzi huo katika hafla iliyohudhuriwa na maelfu ya wafuasi wao katika mji mkuu, Lilongwe.

Kwa upande wa Mutharika na chama chake cha Democratic Progressive mapema mwezi huu waliungana na chama kidogo cha upinzani cha United Democratic Front, kilichoshika nafasi ya nne kwenye uchaguzi wa mwaka jana.

Taifa hilo la kusini mwa Afrika bado halijaorodesha kisa hata kimoja cha COVID.19, lakini kuna wasiwasi kwamba kusambaa kwa virusi vya maradhi hayo vya corona kunaweza kutishia kucheleweshwa zaidi kwa uchaguzi huo.

Hii ni mara ya kwanza kwa matokeo ya uchaguzi wa urais kupingwa kisheria nchini Malawi tangu taifa hilo lilipopata uhuru mwaka 1964 na ni matokeo ya pili ya uchaguzi kupingwa kisheria barani Afrika, baada ya awali matokeo ya uchaguzi wa urais nchini Kenya kubatilishwa.