1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMalawi

Malawi yafanya uchaguzi wa Rais

16 Septemba 2025

Rais wa sasa Lazarus Chakwera anapambana vikali na Rais wa zamani Peter Mutharika. Wagombea wengine 15 akiwemo Rais wa zamani Joyce Banda wanachuana pia katika mbio hizi za kuingia Ikulu ya Malawi.

Lazarus Chakwera | Mahojiano na DW I Josephine Mahachi | Mgombea wa urais
Rais wa Malawi Lazarus Chakwera na mgombea wa urais katika mahojiano na mwandishi wa DW, Josephine Mahachi mjini Berlin siku ya Ijumaa, 23/08/2024Picha: DW

Wananchi wanapiga kura huku mfumuko wa bei za bidhaa muhimu kama chakula ukiongezeka. Jumla wa wagombea 17 akiwemo rais wa sasa Lazarus Chakwera pamoja na Peter Mutharika mwenye historia kubwa nchini Malawi na Rais wa zamani wa nchi hiyo wanachuana kuingia Ikulu.

Hata hivyo Mutharika anaonekana kuwa mpizani mkubwa wa Rais Lazarus Chakwera na kwa mujibu wa sheria za uchaguzi nchini Malawi akikosekana mgombea wa kupata angalau asilimia 50 ya kura zilizopigwa, uchaguzi utarudiwa.

Malawi imekumbwa na mdororo wa kiuchumi tangu mwaka 2020 alipoingia madarakani Rais Lazarus Chakwera ambaye pia ni mchungaji wa zamani wa Kanisa la Assemblies of God kupitia chama chake cha Malawi Congress Party, MCP.

08/06/2019 | Mvulana akinyanua matofali makavu na kuyapeleka kwenye tanuru ambapo yatachomwa ili kupata pesa katika Kijiji cha Jumpha, Mamlaka ya Kimila ya Chitukula huko Lilongwe, katikati mwa Malawi, Juni 7, 2019Picha: AMOS GUMULIRA/AFP

Maisha magumu pia yamesababishwa na maafa yaliyotokana na vimbunga vya mara kwa mara pamoja na ukame ambao umekuwa ukilikumba eneo kubwa la Malawi. Takwimu za mashirika ya kiuchumi na fedha zinaonyesha mfumuko mkubwa wa bei katika kiwango cha asilimia 20 kwa muda wa zaidi ya miaka 3 mfululizo.

Wengi wajitokeza licha ya changamoto za kijamii

Hata hivyo matatizo hayo hayajawazuia wananchi wa Malawi kushiriki uchaguzi huo kama Hamstobe Macnever aliyejitokeza mapema asubuhi kupiga kura "Mgombea ambaye nimempigia kura anapaswa kuhakikisha kuwa vijana wanaajiriwa kuliko ambavyo imekuwa. Nataka kuwaona vijana katika maeneo mengi ya maendeleo.”

Wafuasi wa Chama cha Malawi Congress (MCP) wakicheza ngoma kabla ya kuwasili kwa rais aliye madarakani wa Malawi na mgombea urais wa MCP Lazarus Chakwera wakati wa mkutano wa mwisho wa kampeni kwenye Uwanja wa Civo mjini Lilongwe, Septemba 13, 2025.Picha: Amos Gumulira/AFP/Getty Images

Vituo vya kupigia kura vimefunguliwa asubuhi saa kumi na mbili na vitafungwa saa kumi za jioni saa za Malawi. Maafisa wanaosimamia zoezi hilo wanasema hakujawa na hitilafu yoyote ya kiufundi.

Lakini kwa upande mwingine uchaguzi huu pia unafanyika visa vya ulaji rushwa vikionekana kuwakatisha tamaa wananchi na hata vyama vya upinzani. Rais Chakwera wakati akiingia madarakani mwaka 2020 alikuwa akimtuhumu mtangulizi wake Peter Mutharika kwa ulaji rushwa lakini naye utawala wake umekuwa ukilaumiwa kwa kushindwa kulikabili tatizo hilo.

Wachambuzi wa siasa za Malawi wanasema licha ya kwamba Rais Chakwera aliingia madarakani miaka mitano iliyopita kwa uungwaji mkono lakini kwa sasa hali imebadilika na watu wamepoteza matumaini kwa kiasi kubwa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW