1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiMalawi

Malawi yakabiliwa na mgogoro wa wakimbizi wanaotoka Msumbiji

Bakari Ubena George Mhango
3 Januari 2025

Malawi inakabiliwa na changamoto kubwa ya kuwalisha raia wake pamoja na maelfu ya wakimbizi waliomiminika nchini humo wakikimbia ghasia za baada ya uchaguzi mkuu nchini Msumbiji.

Wakimbizi wa Msumbiji
Wakimbizi wa MsumbijiPicha: Alfredo Zuniga/AFP

Maelfu ya watu wameikimbia Msumbiji na kuelekea nchi jirani ya Malawi, wakitafuta hifadhi kutokana na machafuko ya baada ya uchaguzi mkuu. Hii ni kufuatia hatua ya wiki iliyopita ya Mahakama ya Katiba ya Msumbiji kuthibitisha ushindi wa chama tawala cha Frelimo katika uchaguzi wa mwezi Oktoba mwaka jana.

Upinzani uliyapinga matokeo hayo na kusema yalichakachuliwa ili kukipa ushindi chama tawala na uamuzi huo wa mahakama ya juu nchini humo ulisababisha maandamano makubwa ya vurugu yaliyogubikwa na uharibifu na uporaji.

Soma pia: Kiongozi wa upinzani Msumbuji asema polisi wanahimiza vurugu

Ellen Kaosa ni mmoja wa raia zaidi ya 13,000 wa Msumbiji ambao walitafuta hifadhi katika wilaya ya mpakani ya kusini mwa Malawi ya Nsanje.

Wanawake wa MsumbijiPicha: DW

Yeye na baadhi ya ndugu zake waliondoka Msumbiji siku ambayo mahakama iliidhinisha matokeo hayo ya uchaguzi. Kaosa ameiambia DW kwamba walisafiri kwa kutumia njia hatari.

" Kutoka Msumbiji hadi Malawi, tulitumia njia hatari ikiwa ni pamoja na kuvuka mito ya Shire na Zambezi kwa boti. Hatimaye tuliwasili katika kambi ya watu waliokimbia makazi yao katika kijiji cha Tengani, lakini hali kiutu ni mbaya. Tangu Jumatatu sijala, nina watoto, na wanawake wengine ni wajawazito, wazee na wengine ni watu wenye ulemavu, " alisema Bi Kaosa.

Bi Kaosa ameiambia pia DW kuwa hali ya kibinaadamu ni mbaya katika kambi hiyo ambayo haina vyoo, maji safi au vyandarua na hivyo kuwa hatarini kukabiliwa na miripuko ya magonjwa kama malaria na kipindupindu. Aliongeza kuwa wasamaria wema waliwapa baadhi ya watu kikombe kimoja tu cha uji walipowasili kambini hapo.

Serikali ya Malawi na UNHCR zashirikiana

Mahema ya wakimbizi katika kambi inayosimamiwana shirika la UNHCRPicha: Florian Gaertner/IMAGO

Mkuu wa wilaya ya Nsanje Dominic Mwandira alimwandikia barua Kamishna anayehusika na wakimbizi nchini humo na kumweleza kuwa hali bado ni mbaya, kwani wakimbizi hao kutoka Msumbiji wanahitaji msaada wa dharura wa kibinadamu.

Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wametoa wito wa kuyapa kipaumbele makundi yaliyo hatarini zaidi na wameitaka Malawi na jumuiya ya kimataifa kutoa kipaumbele kwa watoto, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.

Mamlaka za Malawi zimethibitisha kushirikiana na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) ili kutathmini mahitaji ya msaada wa kibinadamu kwa wale wanaoikimbia Msumbiji.

Soma pia: Rais mteule wa Msumbiji atoa wito wa 'kutotumia vurugu'

Kaosa, kama maelfu ya raia wengine ambao wamekimbilia Malawi na Eswatini, ufalme mdogo unaopakana na Msumbiji katika eneo la kusini, wanatarajia usalama na amani vitarejea hivi karibuni ili hatimaye waweze kurejea nchi mwao.

Hata hivyo, Malawi tayari inakabiliana na uhaba wa chakula ili kuweza kuwalisha raia wake, pamoja na wakimbizi wapatao 54,000 - wengi wao ikiwa ni kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda na Burundi - ambao wanaishi katika kambi ya wakimbizi ya Dzaleka katikati mwa Malawi.

(DW)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW