Idadi ya waliokufa Malawi yafikia 326
17 Machi 2023Idadi ya waliokufa kutokana na Kimbunga Freddy baada ya kuikumba Malawi kilipotokea tena kusini mwa bara la Afrika imeongezeka hadi 326, na kufanya jumla ya vifo kufikia zaidi ya 400 tangu Februari. Rais wa taifa hilo Lazarus Chakwera kupitia televisheni amesema vifo vimeongezeka kutoka 225 hadi 326, idadi ya wasio na makazi 183,159.
Chakwera ametoa wito wa msaada wa kimataifa huku waokoaji wakiendelea kutafuta manusura kutokana na mafuriko na maporomoko ya matope yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha juma hili.
Kimbunga hicho kilirejea katika eneo la Bahari ya Hindi, kikakusanya nguvu kutokana na joto la maji na kuanza tena kufanya athari katika maeneo ya watu. Hadi wakati huu kimbunga Freddy kipo katika rekodi ya moja kati ya vimbunga hatari zaidi dunini kwa zingatio la madhila ya Msumbiji. Kwa huko Msumbiji safari hii kimesababisha vifo vya watu 63 na wengine 49,000 kuachwa bila ya makazi.
Soma zaidi:Malawi yatoa wito wa msaada wa kimataifa kufuatia kimbunga Freddy
Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji nae ameomba msaada kwa jumuiya ya kimataifa katika ujenzi mpya wa miundombinu iliyoporomoka. Wataalam wa hali ya hewa wanasema kimbunga hicho ni matokeo ya mabadiliko ya tabia nchi.
Chanzo: AFP