1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaAfrika

Malawi yateketeza chanjo zilizoisha za AstraZeneca

19 Mei 2021

Malawi imeharibu dozi karibu elfu ishirini za chanjo ya covid-19 ya AstraZeneca, licha ya uhakikisho kutoka Umoja wa Afrika na shirika la Afya Duniani WHO, kuwa chanzo hizo zilikuwa salama hadi katikati mwa mwezi Julai.

Malawi vernichtet Covid-19 Impfstoff AstraZeneca
Picha: Amos Gumulira/AFP/Getty Images

Shehena ya chanjo 102,000 iliwasili Machi 26 chini ya mkakati wa Umoja wa Afrika na WHO, na ziliisha muda wake Aprili 13, na kuacha muda wa chini ya wiki tatu tu wa kuzitumia. Malawi ilifanikiwa kutumia karibu asilimia 80 ya chanjo hizo kufikia wakati huo.

Mkurugenzi wa vituo vya kudhibiti na kuzuwia magonjwa Afrika John Nkengasong, aliuambia mkutano wa habari mwezi uliyopita, kwamba dozi hizo zingeweza kutumika hadi Julai 13, kwa msingi wa tathmini zaidi iliyofanywa na watengenezaji - taasis ya Serum ya India.

Waziri wa afya wa Malawi Khumbize Kandodo Chiponda (katikati) akiweka dawa za chanjo ya AstraZeneca zilizoisha muda wake kwenye jaa la taka kwa ajili ya kuchomwa.Picha: Amos Gumulira/AFP/Getty Images

Yeye na WHO pia walizihimiza nchi za Afrika kutotupa chanjo zilizotolewa kama msaada kwao. Hata hivyo serikali ya Malawi ilisema haingeweza kutoa chanjo zilizopitwa na wakati kwa raia wake.

Soma pia: Nchi nyingi maskini bado hazijapokea chanjo ya corona

Waziri wa afya wa Malawi Khumbize Chaponda, amesema wamechoma chanjo hizo kwa sababu kulingana na sera ya serikali, hakuna chanjo iliyopitwa na wakati imewahi kutumika.

"Tunazo taarifa kwamba tamko lilikuja kutoka WHO ambalo lilisema ikiwa imeisha muda wake bado tungeweza kuitumia. Lakini kama taifa, tayari tulikuwa tumefanya uamuzi kwamba hatutotumia chanjo yoyote iliyopitwa na wakati," alisema waziri Chaponda.

Ruksa ya kutumia chanjo baada ya muda

Afisa wa kituo cha kudhibiti na kuzuwia magonjwa Afrika CDC alikataa kuzungumzia suala hilo. Taasisi ya Serum India pia haikujibu mara moja ombi la kutoa tamko.

Mamlaka ya udhibiti wa dawa ya India mnamo mwezi Machi iliruhusu chanjo ya AstraZeneca iliyotengenezwa na Serum, kutumika kwa hadi miezi tisa kuanzia tarehe ya kutenegenezwa kwake, tofauti na ruhusa ya awali ya miezi sita.

Shehena ya chanjo inayotolewa chini ya mpango wa kimataifa wa Covax.Picha: Mamyrael/AFP

Sudan Kusini imetenga dozi 59,000 zilizotolewa na Umoja wa Afrika, na haizitumii kwa sababu ya masuala sawa ya kuisha muda wa matumizi. Wizara ya afya ya Malawi imesema nchi hiyo imetoa dozi 335,232 za chanjo kufikia Mei 18, na kurikodi maambukizi 34,231 ya Covid na vifo 1,153.

Soma pia: Kenya yaagiza chanjo zaidi milioni 30 za corona

Mataifa ya Afrika yamepambana kupata chanjo za kutosha kutoa kwa watu wengi, na mengi yanategemea msaada kutoka mpango wa kimataifa wa Covax, unaoongozwa kwa pamoja na WHO na washirika, ukiwemo muungano wa chanjo wa Gavi.

Austria wiki hii imekuwa nchi ya tatu ya Ulaya kuachana na chanjo ya AstraZeneca, baada ya Norway na Denmark kutupilia mbali matumizi yake kutokana na visa vya nadra vya kuganda kwa damu miongoni mwa watu waliopatiwa chanjo hiyo.

Chanzo: Mashirika