1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Malema avutia wapigakura kuchagua EFF

Angela Mdungu
7 Mei 2019

Wakati Afrika Kusini ikielekea kwenye uchaguzi mkuu kiongozi wa chama cha upinzani cha Economic Freedom Fighters EFF Julius Malema anatumia hoja ya udhaifu wa chama tawala cha ANC kuvutia wapigakura kuchagua chama chake.

Südafrika - Wahl / Vorsitzender der Partei für wirtschaftliche Freiheitskämpfer (EFF), Julius Malema
Picha: picture-alliance/M. Safodien

 Kampeni za lala salama zinaendelea nchini Afika ya kusini kuelekea uchaguzi. Katika kampeni za uchaguzi huo  Julius Malema, kiongozi wa Chama cha upinzani cha Economic Freedom Fighters, EFF, amekuwa akiwashawishi wananchi kukichagua chama chake akitumia hoja ya udhaifu wa Chama cha African National Congress, ANC, chini ya Rais Cyril Ramaphosa kushindwa kuondoa umasikini na kuwakumbatia wazungu.

Kama ilivyo kwa mtu yeyote anayetaka kuvutia umati, mwanasiasa Julius Malema anafahamu namna ya kutia watu shauku. Anawaacha wasubiri na kisha anawaambia hasa kile wanachotaka kusikia. Kwa muda wa saa mbili wafuasi wake wakiwa wamebeba mabango yenye kauli mbiu zenye ujumbe wa kimageuzi, muziki mkubwa na hotuba za maandalizi katika uwanja wa michezo katika kitongoji cha Alexandra mjini Johannesburg.

Kiongozi wa chama cha EFF Julius Malema akihutubia mkutano wakati wa uzinduzi wa ilani ya chama hicho mjini Pretoria, Februari 2, 2019.Picha: Getty Images/AFP/P. Magakoe

Hatimaye kiongozi wao anatokea, akiwa na gari la kijerumani na kupita jukwaani akipokea heshima. Umati wa watu unasikika ukisema ''Songa mbele kuelekea ushindi 2019-mbele'', ikiwa ni siku kadhaa kabla ya uchaguzi utakaofanyika Jumatano ya tarehe nane mwezi Mei. Malema ambaye amejitengenezea utambulisho wake kama ''Amiri jeshi mkuu'' wa wapigania uhuru wa uchumi katika chama chake cha EFF akiwa amevalia sare ya chama hicho na kofia nyekundu alikuwa amezungukwa na kundi la walinzi wake wanaojulikana kama watetezi wa mapinduzi.

Katika mkutano wake huko Alexandra, Malema amewaambia wafuasi wake ni lazima waichukue ardhi kutoka mikononi mwa wazungu na kuwapa watu wa eneo hilo ili wagawane utajiri wa nchi hiyo. 

 ''Kuna fedha nyingi hapa Afrika kusini ambazo zinapotezwa na wanasiasa. Hebu tuokoe pesa. Mnataka kuzifanyia nini? Ninataka kuwapa akina bibi, nataka kuwapa watoto fedha kutoka katika mifuko ya wanasiasa,'' alisema katika mkutano huo wa Alexandra.

Mkombozi wa wanyonge?

Mmoja wa wafuasi wa siasa za Malema Steven Chauke mwenye umri wa miaka 58 ambaye hana ajira kwa miaka 16 anasema Malema ndiye anayeweza kusikia maumivu ya watu na ndiye pekee anaweza kuwasaidia. Anasema kwa miaka 25 chama tawala ANC hakijawahi kufanya kazi kwa ajili ya raia bali kwa maslahi binafsi.

EFF Chama cha tatu kwa ukubwa cha mrengo wa kushoto nchini Afrika ya Kusini, kinatumai kupata ushindi katika uchaguzi ikiwa chama tawala cha ANC kitalipa gharama ya kuchelewa katika juhudi za kupunguza umasikini tangu kukomeshwa kwa utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika ya Kusini  mwaka 1994.

Wafuasi wa chama cha EFF wakiandamana nje ya bunge la Afrika Kusini mjini Cape Town.Picha: picture-alliance/dpa/Nic Bothma

Katika eneo la Alexandra alipofanya mkutano Julius Malema, ni mji wenye msongamano na umasikini huku ukiwa karibu na mji tajiri wa Sandton, ulio muhimu kwa uchumi wa Jonnesburg. Alexandra umeathiriwa vibaya na kushindwa kwa utawala wa ANC kwa ukosefu wa ajira,  huduma duni kwa umma, uhalifu na rushwa. Masuala haya yamemfanya Malema, ambaye hapo awali aliwahi kuwa kiongozi wa vijana wa ANC kuanzisha chama chake mwaka 2013 na kukiimarisha ndani ya miaka kadhaa na kuwa tishio kwa vyama vingine vya siasa nchini Afrika kusini.   

Malema mwenye umri wa miaka 38 anakusudia kumvaa Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa ambaye pia ni Rais wa chama cha ANC kutokana na mateso ya kiuchumi, na tuhuma za rushwa zinzokikabili chama tawala pamoja na tuhuma za Rais Ramaphosa kuwapendelea wazungu ambao bado wanamiliki utajiri mkubwa.

Hata hivyo wakati akizungumza na shirika la habari la AFP Malema amejitetea kwa kusema hana tatizo na wazungu bali tatizo lake ni upendeleo maalumu wanaopewa wazungu na iwapo chama chake kitashika dola, hakuna mzungu atakayeuawa ila itabidi wajishushe na kuwa sawa na watu wengine.

chanzo: afpe

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW