1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Malema mwerevu mbinu za siasa

25 Aprili 2012

Chama tawala Afrika Kusini ANC kinataka kumuweka katika kaburi la sahau aliyekuwa Rais wa Umoja wa Vijana wa chama hicho Julius Malema.

Julius Malema Kiongozi wa zamani wa Umoja wa Vijana wa ANC anayetazawa kuwa na mbinu za kisiasa
Julius Malema Kiongozi wa zamani wa Umoja wa Vijana wa ANC anayetazamwa kuwa na mbinu za kisiasaPicha: AP

Hilo linatazamwa halitofanikiwa kwani linaweza kukigarimu chama hicho na Rais Jacob Zuma katika harakati zake za kuwa Rais wa ANC na wa Nchi hiyo 2014.

Kiongozi kijana ambaye rufaa yake imekataliwa kwa tuhuma za kuleta mgawanyiko ndani ya chama hicho anatazamwa kuwa na kundi kubwa katika chama hicho ambalo linamuunga mkono na linaweza kufanya na kusema yale aliyokuwa akitenda Malema pasi na kuwapo yeye chamani.

Wachambuzi wa mambo wanaona kuwa ndani ya ANC kuna vijana wengi wenye msimamo huo na watasonga mbele na tabia hiyo ambayo imeonekana kuwa kero kwa watawala wa ANC.

Utabiri wa wachambuzi

Steven Friedman mchambuzi wa masuala ya kisiasa anasema nafasi ya Malema kwa sasa ni kubwa kwani wale waliokuwa wanamuona kuwa mtetezi na mtu muhimu kwao watampigania kufa na kupona katika mkutano wa disemba mwaka huu ambapo uchaguzi wa rais wa Chama hicho utafanyika.

Hoja hii pia inaungwa mkono na mwandishi wa Kitabu cha wasifu Kiongozi huyu, Fiona Forde. Akizungumza na Shirika la Habari la AFP, Forde amesema sasa si wakati wa kusema kuwa Malema ameshindwa, bali tamati ya yote ni Disemba.

Mwandishi huyu anaongeza kuwa Malema ni mwerevu mno wa mbinu za kisiasa. Ametoa mfano katika uchaguzi wa rais wa ANC mwaka 2007 Malema alisema bayana kuwa yu radhi kufa kuliko kumuacha aliyekuwa Rais wa ANC na Afrika Kusini wakati huo, Thabo Mbeki, anachanguliwa rais wa chama hicho. Hivyo ndiyo ilivyokuwa na Jacob Zuma akashinda uchaguzi na kuwa Rais wa ANC na baadae kuiongoza Afrika Kusini.

Mwandishi huyo anasema yale aliyokuwa anatuhumiwa Mbeki sasa yapo kwa Zuma kwani ameshindwa kuyatatua matatizo ya Waafrika Kusini.

Hapo awali kauli ya Malema mwenyewe inafanana na kile anachokisema mwandishi huyu kuwa hatima yake ipo kwa wanachama wa ANC ambao ndio watakaoshiriki mkutano wa disemba.

Rais wa zamani wa ANC na Afrika Kusini Thabo MbekiPicha: picture-alliance /dpa

Ujumbe wa Malema kwenye simu ya mkononi

Mpaka sasa hakuna taarifa rasmi juu ya kauli ya Malema tangu kufutwa uanachama, lakini kulingana na gazeti la Star, simu yake ya mkononi imekuwa na ujumbe mzito wa maneno. Kwa wale wanaompingia, kumekuwa na maamkizi yanayosema: "Hakuna kushindwa, hakuna kujisalimisha, ushindi ni lazima!"

Ujumbe huo unamalizia kwa maelezo kuwa: "Hatimaye tutasahau maneno yaliyosemwa na maadui zetu, lakini tutakumbuka ukimya wa marafiki zetu wakati tulipokuwa tabuni."

Malema na sera ya ubinafsishaji

Msemaji wa ANC Jackson Mthembu amesema suala la Malema limewachukua miezi tisa kuamua, lakini sasa wamefikia hitimisho, japokuwa ni maamuzi magumu na ya uchungu. Amesema maamuzi hayo yamefikiwa kwa nia moja tu ya kulinda chama chao.

Rais wa sasa wa ANC na Afrika Kusini Jacob ZumaPicha: AP

Malema anaonekana kuwa mtetezi wa Waafrika Kusini masikini, ambao mpaka sasa, miaka 18 ya uhuru kutoka kwa utawala wa weupe wachache uliondoka madarakani mwaka 1994, hawajaonja matunda ya uhuru wao kwani asilimia 40 ya wananchi wote ni masikini wa kutupwa huku asilimia 24 hawana ajira.

Malema alishauri kubinafsishwa kwa migodi, mabenki na kutaifishwa kwa mashamba yote yanayomilikiwa na wazungu , huo ukiwa ni miongoni mwa misimamo ya ANC hapo awali. Pia ahadi mojawapo ya Rais Jacob Zuma kabla ya kuwa rais ilikuwa ni kuhakikisha angewasaidia wanyonge, huku sasa akijikita katika soko huria kuondoa upungufu wa ajira na mabilioni ya fedha yanatumika kwa miradi mikubwa.

Mwandishi: Adeladius Makwega/AFPE

Mhariri: Mohammed Khelef