1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMali

Onyo latolewa kuhusu uingiliaji wa kijeshi nchini Niger

1 Agosti 2023

Serikali za kijeshi za Mali na Burkina Faso zimeonya kuwa uingiliaji wowote kijeshi nchini Niger utazingatiwa kuwa "tangazo la vita" pia kwa nchi zao.

Jenerali Abdourahmane Tiani, ambaye alitangazwa kuwa mkuu mpya wa nchi ya Niger na viongozi wa mapinduzi, akiwasili kukutana na mawaziri huko Niamey, Niger Julai 28, 2023.
Jenerali Abdourahmane Tiani, aliyetangazwa kuwa mkuu mpya wa nchi ya Niger na viongozi wa mapinduzi, akiwasili kukutana na mawaziri huko Niamey, Niger Julai 28, 2023.Picha: Balima Boureima/REUTERS

Nchi hizo zimeonya kuhusu madhara makubwa ya uingiliaji kijeshi nchini Niger, ambayo yanaweza kuidhoofisha kanda nzima. Aidha zimesema zinakataa kutekeleza kile zililichoita vikwazo haramu na vya kikatili dhidi ya watu na maafisa wa Niger. Utawala mpya wa kijeshi nchini Niger umeituhumu Ufaransa kwa kutaka kuingilia kijeshi ili kumrejesha madarakani Mohamed Bazoum.

Wanajeshi wa Niger waishtumu Ufaransa

Wanajeshi hao waasi kupitia Kanali Amadou Abdramane waliishambulia Paris kwenye televisheni ya taifa wakisema kuwa Ufaransa, kwa ushirikiano wa baadhi ya watu wa Niger, ilifanya mkutano katika makao makuu ya Jeshi la Niger la Ulinzi wa Taifa ili kupata vibali muhimu vya kisiasa na kijeshi. Ufaransa ilijibu huku Waziri wa Mambo ya Kigeni Catherine Colonna akikanusha tuhuma hizo na kuongeza kuwa bado inawezekana kumrejesha Bazoum madarakani.