1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mali na Ivory Coast zajaribu kutatua mivutano yao

23 Desemba 2022

Mali inawashikilia wanajeshi 46 wa Ivory Coast iliowafungulia mashtaka ikiwatuhumu ni mamluki walioingia kwenye ardhi ya nchi yake

Elfenbeinküste Soldaten
Picha: ISSOUF SANOGO/AFP/Getty Images

Ujumbe wa Ivory Coast uliingia nchini Mali Alhamisi ukiongozwa na Tene Birahima Outtarra ambaye ametowa tamko kuhusu suala hilo la wanajeshi 46 wa nchi yake kushikiliwa na utawala wa Mali, akisema ni suala ambalo linatafutiwa ufumbuzi na wanachoweza kusema ni kwamba ziara yao nchini Mali imezaa matunda. 

Brahima amesema ilikuweko hali ya kutoelewana baina ya jamhuri hizo mbili, Mali na Ivory Coast, miezi michache iliyopita na kwamba limekuwa jambo zuri wamekutana na kujadili.

Mvutano kati ya nchi hizo ulizuka Julai 10 pale wanajeshi 49 wa Ivory Coast walipokamatwa baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Mali, baadae watatu waliachiwa huru na 46 wakazuiliwa. Wanajeshi hao wa Ivory Coast na Umoja wa Mataifa kimsingi walipelekwa Mali katika utaratibu wa kawaida wa kwenda kukisaidia kikosi cha  Ujerumani ambacho ni sehemu ya ujumbe wa  kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Mali.

Lakini serikali mjini Bamako imetuhumu kwamba ni mamluki na mnamo mwezi Agosti walifunguliwa mashtaka ya kutaka kuuhujumu usalama wa nchi hiyo.

Mvutano huu uliongezeka na mwezi uliopita Ivory Coast ikasema itawaondowa wanajeshi wake katika ujumbe huo wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Mali, MINUSMA. Lakini pia Desemba 4, mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika, ECOWAS,  ukaitaka Mali kuwaachia huru wanajeshi hao kufikia mwaka mpya kinyume na hivyo itawekewa vikwazo vipya

Picha: IVORY COAST PRESIDENTIAL PRESS SERVICE/REUTERS

.Mali kusitisha mizunguko ya mpango wa Umoja wa Mataifa wa MINUSMA

Kwahivyo ziara hiyo ya ujumbe kutoka Ivory Coast,mjini Bamako ni hatua ya kujaribu kuutafutia ufumbuzi mvutano huu. Waziri wa mambo ya nje wa Mali Abdoulaye Diop amesema wameona kuna dhamira kwa pande zote ya kushirikiana kumaliza tatizo hili kwa kuuendeleza uhusiano uliokuweko baina ya nchi hizo mbili. Diop pia amesema mazungumzo yao yamechangia kusainiwa kwa mkataba wa maelewano kuimarisha amani na kushirikiana kuimarisha mahusiano ya kirafiki kati ya nchi hizo mbili.

 Ujumbe wa Ivory Coast utakutana na kiongozi wa kijeshi Kanali Assimi Goita na kuzungumza pamoja na wanachama wengine wa seriali. Lakini wakati huohuo Mali yenyewe inakabiliwa na matatizo mengine ya ndani jana makundi takriban yote ya wanamgambo ambayo yalisaini makubaliano ya amani ya mwaka 2015 yalijiondowa kwenye makubaliano hayo yakilalamika kwamba utawala wa kijeshi hauna nia ya kisiasa ya kuendeleza makubaliano hayo.

Picha: Habibou Kouyate/AFP/Getty Images

Muungano wa Awazad ambao unashikiliwa na idadi kubwa ya Watuareg na ambao ulikuwa kwenye mapambano kwa muda mrefu na serikali ya Bamako kabla ya kufikiwa makubaliano ya Algiers na makundi mengine takriban yote ya wanamgambo wa kaskazini mwa Mali wamejiondowa katika makubaliano ya utekelezaji mkataba huo.Makundi ya wanamgambo ya itikadi kali yazusha wasiwasi Afrika Magharibi

Taarifa ya makundi hayo imesema itashikilia msimamo huo mpaka utakapofanyika mkutano utakaosimamiwa na jumuiya ya Kimataifa na msuluhishi huru na utakaoamuwa kuhusu mustakabali wa makubaliano hayo. Itakumbukwa kwamba eneo la Kaskazini mwa Mali muongo mmoja uliopita liliharibiwa na vita baada ya wanamgambo wa Tuareg kuanzisha harakati za kudai uhuru au kujitenga na Bamako na  kuwa na mamlaka yao.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW