Mali, Senegal zatinga robo fainali AFCON-2025
5 Januari 2026
Mali imejiunga na Senegal katika robo fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika – AFCON 2025 baada ya kutoka nyuma na kuipiga Tunisia kwa mikwaju ya penalti.
Kipindi cha kwanza kilichojaa purukushani kilishuhudia kadi nne za njano zikitolewa na mwamuzi kabla ya Woyo Coulibaly kuoneshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja kunako dakika ya 26. Alimtendea madhambi Hannibal Mejbri na katika mechi iliyokuwa na fursa chache, Tunisia hatimaye ilifunga bao kunako dakika ya 88 wakati krosi maridadi kabisa ya Elias Saad ilipotiwa wavumi kupitia kichwa cha Firas Chaouat.
Hata hivyo, mambo yalipamba moto wakati Mali walipewa mkwaju wa penalty baada ya Yassine Meriah kuunawa mpira kwenye sanduku na Lassine Sinayoko akasukuma wavuni katika dakika ya sita ya muda wa majeruhi na kufanya mambo kuwa 1 – 1 katika muda wa kawaida wa mchezo huo wa AFCON.
Katika muda wa nyongeza, Tunisia walifunga bao lililofutwa kwa kuwa lilikuwa la kuotea na mpambano huo ukaingia hadi mikwaju ya penalti. Kipa wa Mali anayechezea klabu ya Tanzania ya Yanga Djigui Diarra alipangua mikwaju miwili kabla ya El Bilal Toure kufunga mkwaju wake na kuwapa Mali ushindi wa 3 -2 uliowapeleka robo fainali.
Senegal yaifurusha Sudan
Awali, mabao mawili ya Pape Gueye yaliisaidia Senegal kutoka nyuma na kuichapa Sudan 3 – 1 na kutinga robo fainali Jumamosi.
Sudan ilijiweka kifua mbele mjini Tanger dakika sita tu baada ya mechi kuanza wakati Aamir Abdallah alimbwaga kipa Edouard Mendy kwa kombora safi. Lakini Gueye aliisawazishia Senegal kunako dakika ya 29 kwa kusukuma wavuni shuti safi pembeni mwa eneo la penalty baada ya kaundaliwa pasi na Sadio Mane.
Ismaila Sarr alidhani ameipatia penalti Senegal dakika za mwisho mwisho za kipindi cha kwanza alakini alikuwa ameotea wakati alipopata nafasi ya kuingia langoni, na kisha akafunga bao lililofutwa kwa kuwa alikuwa ameotea tena.
Hata hivyo, Gueye alifunga bao kunako dakika ya kwanza ya kipindi cha pili, kwa kuunganisha pasi ya Nocolas Jackson, na Ibrahim Mbaye, kinda wa Paris Saint-Germain akatokea benchi na kufunga bao safi la kuihakikishia ushindi Senegal kunako dakika ya 77.