Mali yakubaliana na waasi wa Tuareg
25 Juni 2013Makubaliano haya ya sasa ya amani ambayo yamefikiwa baada ya vuta nikuvute iliyodumu kwa zaidi ya siku 10, yatawezesha vikosi vya jeshi la Mali kuingia katika mji unaoshikiliwa na waasi wa Tuareg wa Kidal, huko maeneo ya kaskazini mashariki ili kufanikisha uwezekano wa kufanyika kwa uchaguzi uliopangwa kufanyika Julai 28 mwaka huu.
Pande zote mbili zimekubaliana kuacha uhasama na kwamba mazungumzo ya muda mrefu ya amani yatafanyika baada ya kumalizika uchaguzi huo. Katika mkutano uliofanyika mjini Ouagadougou, Burkina Faso, Waziri wa utawala wa taifa, Mousa Sinko Coulibaly, ametia saini makubaliano hayo pamoja na wawakilishi wawili wa harakati za Watuareg.
Hatua ya kuachana na chuki
Mahamadou Djeri Maiga, makamo wa rais wa chama cha kitaifa cha harakati za ukombozi cha Azawad, kutoka upande wa Tuareg, amesema makubaliano hayo ni fursa ya kubadili ukurasa wa chuki.
Kumekuwa na hali ya kutoaminiana kati ya serikali ya Mali na waasi wa Tuareg, ambao walianzisha vuguvu dhidi ya serikali nchini humo sambamba na makundi ya wapiganaji wa Kiislamu yenye mfungamano na Al-Qaeda. Majeshi ya Ufaransa yaliingilia katika vuguvugu hilo na kufanikiwa kuzuiwia wanamgambo hao kusonga mbele kuelekea katika maeneo ya mji mkuu wa Mali.
Ufaransa yasifu mafanikio hayo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Laurent Fabius amesema makubaliano hayo yanawakalisha mafanikio makubwa katika mgogoro uliopo nchini Mali. Aidha ameongeza kwa kuwatolewa wito raia wa Mali kuungana kwa lengo moja kutekeleza makubaliano hayo kwa maslahi ya taifa.
Mkuu wa Sera za Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton amesema makubaliano hayo yana umuhimu mkubwa kihistoria huku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akiyakaribisha makubaliano hayo kwa kuzitaka pande zote mbili kuanza kwa pamoja utekelezaji wake.
Lakini mjumbe wa umoja huo kwa Mali, Bert Koenders amesema makubaliano hayo ni hatua ya kwanza. Amefafanua kwamba mazungumzo muhimu kuhusu kushughulikia masuala ya usalama, uwekaji wa utawala na huduma muhimu katika mji wa Kidal bado hayajaanza.
Mdau mwingine kuhusu hali ya Mali, Robert Piper, ambae anaratibu ofisi ya misaada ya kiutu ya Umoja wa Mataifa katika kanda ya Sahel amesema Mali bado inakabiliwa na matatizo makubwa. Mratibu huyo ameonya kuwa matatizo ya kiutu yanaweza kutapakaa nchini kote na kuongeza watu wa kaskazini wapo katika hatari zaidi.
Katika mkutano maalumu kuhusu kusadia Mali uliofanyika mwaka uliopita. zaidi ya euro milioni 133 zilikusanywa kati ya kiwango cha euro milioni 410 kilichokusudiwa. Mratibu huyo wa misaada ya kiutu wa Umoja wa Mataifa ametahadharisha kiasi hicho cha pesa lazima kipatikane kabla hali haijawa mbaya zaidi.
Mwandishi: Sudi Mnette AFP
Mhariri:Josephat Charo