1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mali yasimamishwa uanachama wa ECOWAS

31 Mei 2021

Viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi ECOWAS wametangaza kusimamisha uachama wa Mali baada ya jeshi la nchi hiyo kufanya mapinduzi ya pili ndani ya miezi tisa.

Ghana ECOWAS | Nana Akufo-Addo
Picha: AFP/N. Dennis

Uamuzi huo wa kuchukulia hatua dhidi ya Mali umefikiwa na kutangazwa wakati wa mkutano wa dharura wa kanda ya ECOWAS uliofanyika jana Jumapili mjini Accra nchini Ghana.

Viongozi wakuu 10 na mawaziri wa mambo ya kigeni 3 wa mataifa wanachama wa Ecowas walihudhuria mkutano huo na katika tamko la mwisho wamesema wana wasiwasi mkubwa na hali ya usalama kwenye eneo la Afrika Magharibi kutokana na kile kinachoendelea nchini Mali.

Kupitia taarifa kuhusu maazimio ya mkutano huo iliyowasilishwa na waziri wa mambo ya kigeni wa Ghana Shirley Attorkor uanachama wa Mali utasitishwa hadi Februari 2022 ambao ni muda uliopangwa kwa taifa hilo kufanya uchaguzi na madaraka kukabidhiwa kwa serikali ya kiraia itakayochaguliwa kidemokrasia.

Serikali ya mpito ina muda wa hadi Februari 2022

Viongozi hao wa ECOWAS wameutumia mkutano wao kulaani kwa matamshi makali mapinduzi ya kijeshi yaliyofanywa Jumatatu iliyopita nchini Mali na kutoa rai ya kurejeshwa kwa utawala wa kiraia haraka iwezekanavyo.

Kanali Assimi Goita ndiye kiongozi wa mpito wa Mali baada ya jeshi kutwaa madarakaPicha: AP Photo/picture alliance

Zaidi kuhusu hilo waziri wa mambo ya kigeni wa Ghana Shirley Attorkor amesema ''Moja ya maamuzi ya wakuu wa nchi ni kwamba ni lazima katika siku chache zijazo wateue waziri mkuu asiye mwanajeshi atakayeunda serikali.

Serikali ya mpito kwa kipindi kilichosalia, kwa maana wamebakisha miezi nane tu, ambao ni muda wa mwisho waliopewa"

Muda huo wa mwisho ndiyo mnamo Februari 2022 kutakapoitishwa uchaguzi na ECOWAS imesema viongozi watakaounda serikali ya sasa ya mpito hawataruhusiwa kuwania katika uchaguzi huo wa mwakani.

Licha ya kupendekeza hatua kadha za kuchukuliwa hivi sasa, Jumuiya ya ECOWAS haijasita kulinyooshea kidole cha lawama jeshi la Mali kwa kurejesha nyuma juhudi za kuleta uthabiti kwenye taifa hilo.

Juhudi hizo ni pamoja na makubaliano yaliyofikiwa Septemba mwaka uliopita, kiasi mwezi mmoja tangu jeshi lilipofanya mapinduzi ya kwanza yaliyoongozwa na Kanali Assimi Goita ambaye sasa ndiye rais wa mpito wa Mali baada ya kufanyika mapinduzi mengine wiki iliyopita.

ECOWAS: Viongozi wanaoshikiliwa waachiwe 

Kwa miaka mingi hali ya usalama nchini Mali imekuwa tetePicha: Yacouba Cisse/AP/dpa/picture alliance

Taarifa ya ECOWAS pia imetoa wito wa kuachiwa haraka kwa viongozi wanaoshikiliwa na Jeshi.

Viongozi hao wanajumuisha rais wa mpito aliyelazimishwa na jeshi kuondoka madarakani Bah N'Daw na waziri mkuu wake Moctar Ouane ambao wote wamewekwa kwenye kizuizi cha nyumbani tangu kutokea mapinduzi.

Pamoja na hali ya wasiwasi inayoendelea, viongozi wa ECOWAS wamehimiza wadau wa kimataifa ikiwemo Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya kuendelea kuiunga mkono Mali kufanikisha utekelezaji wa kipindi cha mpito.

Mapinduzi ya kijeshi ya wiki iliyopita mabayo yalichochewa na mabadiliko yaliyofanywa na rais wa mpito ambayo yaliwaondoa makamanda wa jeshi kwenye nyadhifa kadhaa yamelaaniwa na Jumuiya ya Kimataifa na kufufua wasiwasi mkubwa juu ya usalama wa Mali na kanda nzima ya Sahel.