Malumbano ya kidiplomasia kuhusu Snowden yachacha
28 Juni 2013Malumbano ya kidiplomasia kufuatia kisa cha Edward Snowden, afisa wa zamani wa shirika la usalama wa taifa nchini Marekani, yamezidi kuchacha leo wakati utawala wa mjini Washington ulipoinyoshea kidole cha lawama serikali ya Hong Kong kwa kufanya hila ilipomruhusu Snowden kuondoka nchini humo. Hatima ya Snowden mwenyewe bado haijajulikana kwa siku ya sita leo huku akibakia kukwama katika uwanja wa ndege wa Sheremetyevo, katika mji mkuu wa Urusi, Moscow.
Afisa wa Urusi anayelifuatilia kwa karibu suala la Snowden ameliambia shirika la habari la Interfax leo hii kwamba Marekani ilifanya makusudi kuitosa Urusi katika kilindi cha maji, akidai maafisa wa mjini Washington hawakuwapa taarifa kwamba pasipoti ya afisa huyo ilikuwa imefutwa na alikuwa amepigwa marufuku asisafiri. Marekani inamtaka Snowden kwa kufichua habari juu ya mipango yake ya kudokoa taarifa.
Venezuela iko tayari kumkaribisha Snowden
Kwa upande mwingine, rais wa Venezuela, Nicolas Maduro, amesisitiza nchi yake iko tayari kumpa Snowden kibali cha uhamiaji, akimsifu kama kijana shujaa. "Kama kijana huyo anahitaji ulinzi wa kibinaadamu na anaamini anaweza kuja Venezuela, basi Venezuela iko tayari kumlinda kijana huyu shupavu kwa njia ya kibinaadamu ili walimwengu wajue ukweli na sakata lake liishe," alisema Maduro. Maduro ameitaja hatua ya Snowden kama 'mapinduzi ya ukweli' na inayoashiria kitu kinachoendelea miongoni mwa vijana wa Marekani.
Ecuador inaonekana kuwa taifa ambalo Snowden anataka kwenda, lakini rais wa nchi hiyo, Rafael Correa, amesema serikali yake bado haijaizingatia kesi ya afisa huyo wa zamani wa ujasusi. "Hali ni ngumu kwa sababu ili kulishughulikia ombi la ukimbizi la Edward Snowden, atatakiwa kuwa katika ubalozi wa Ecuador au himaya ya Ecuador. Na ili hilo lifanyike, nchi inatakiwa kumruhusu aingie katika ardhi yake, jambo ambalo halijafanyika. Bwana Snowden yuko katika hali ngumu na hatujui sakata hili litatatuliwa vipi."
Wakati huo huo, Lonie Snowden, babake Edward Snowden, amesema leo kuwa mwanawe anaweza kurejea Marekani kama masharti fulani yatatimizwa. Akihojiwa na shirika la habari la Marekani, NBC, baba huyo amesema miongoni mwa masharti hayo huenda yakajumuisha kutomtia mbaroni kijana wake kabla kufunguliwa mashitaka, kutomuweka chini ya sheria ya kuzuiliwa na kumruhusu achague ni wapi anakotaka kesi yake isikilizwe.
Sakata lengine laanza
Wakati hayo yakiarifiwa, jenerali mstaafu wa jeshi la Marekani, James Cartwright, analengwa katika uchunguzi wa wizara ya sheria ya nchi hiyo kuhusiana na kuvujisha taarifa za siri juu ya shambulizi la kirusi cha kompyuta aina ya Stuxnet dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran mnamo mwaka 2010. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya jana (27.06.2013) ya shirika la utangazaji la NBC, likivinukuu vyanzo vya sheria visivyojulikana.
Shirika la NBC limesema Cartwright, aliyewahi kuwa afisa aliyeshikilia nafasi ya pili katika jeshi la Marekani, anachunguzwa kuhusiana na taarifa hizo zilizovuja kuhusu kirusi cha kompyuta, kilichokwamisha kwa muda nyenzo 1,000 zinazotumiwa na Iran kurutubishia madini ya urani na kuutatiza mpango wa nyuklia wa Iran. Cartwright, jenerali mstaafu mwenye nyota nne, alikuwa naibu mwenyekiti wa kamati ya wanadhimu wa jeshi la Marekani.
Mwandishi: Josephat Charo/RTRE/AFPE
Mhariri: Saumu Yusuf Saumu