1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Malumbano ya ndani yaiandama serikali ya Merz

5 Mei 2026

Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz alichukua madaraka kwa kuahidi kuirejesha Ujerumani katika hali yake ya kusimama imara kisiasa baada ya kipindi cha misukosuko, kuimarisha hadhi ya nchi na kuanzisha uchumi unaodorora.

Deutschland Hannover 2026 | Kansela  Friedrich Merz
Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz Picha: Martin Meissner/AP Photo/picture alliance

Hata hivyo, ikiwa kesho Jumatano (06.05.2026) inatimia mwaka mmoja madarakani, serikali yake ya muungano umekumbwa na malumbano ya ndani, uchumi wa nchi bado unasuasua na baadhi ya wachambuzi  tayari wanatabiri kwamba hatomaliza muhula wake madaraka.

Katika mwaka wake wa kwanza madarakani, Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz alikabiliwa na changamoto kubwa, huku umaarufu wa serikali yake ukishuka na vyama vya siasa kali vikizidi kupata uungwaji mkono. Licha ya ahadi yake ya kuimarisha siasa za mrengo wa kati, hali inaonekana kwenda kinyume na matarajio yake.

Chama cha mrengo mkali wa kulia cha Alternative for Germany (AfD) kimeendelea kuimarika, kikipata uungwaji mkono mkubwa katika tafiti za maoni. Baada ya kushika nafasi ya pili katika uchaguzi wa 2025 kwa asilimia 20.8, sasa chama hicho kinakaribia asilimia 28, kiwango kinacholingana na kile kilichopatikana na muungano wa Merz wa CDU/CSU.

Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz Picha: Yiannis Kourtoglou/REUTERS

Wachambuzi wa siasa wanasema ongezeko hilo linaashiria mabadiliko ya kina katika siasa za Ujerumani, ambapo vyama vya jadi vinapoteza mvuto wao. Kwa mujibu wa mtaalamu wa siasa Benjamin Hoehne, AfD sasa ina wafuasi wa kudummerz changamoto afdu wasiobadilika kirahisi kulingana na matukio ya kisiasa.

Vyama vya CDU/CSU na SPD vinaendelea kuporomoka 

Kwa upande mwingine, vyama vikuu vya jadi kama CDU/CSU na SPD vinaendelea kuporomoka katika kura za maoni. CDU iko chini ya asilimia 25 huku SPD ikishuka chini ya asilimia 15, hali inayoonyesha kupungua kwa ushawishi wa vyama vya mrengo wa kati vilivyotawala siasa za Ujerumani kwa miongo kadhaa.

Hali hiyo inaonekana zaidi katika majimbo ya mashariki mwa Ujerumani, ambapo AfD inaongoza na huenda ikashinda kwa wingi katika uchaguzi wa majimbo unaotarajiwa kufanyika mwezi Septemba. Hata katika maeneo ya magharibi yaliyoendelea zaidi kiuchumi, chama hicho pia kinaendelea kupata nguvu.

Vyama vikuu vya jadi kama CDU/CSU na SPD vinaendelea kuporomoka katika kura za maoni. Picha: Frederic Kern/Future Image/IMAGO

Ndani ya serikali ya muungano, mvutano kati ya muungano wa CDU/CSU na chama cha SPD umeendelea kuongezeka, jambo linalokwamisha juhudi za kufanya mageuzi muhimu. Migogoro hiyo imekuwa ikichelewesha maamuzi muhimu, hasa katika wakati ambapo uchumi wa nchi unahitaji hatua za haraka za kuimarishwa.

Katika juhudi za kupunguza mvuto wa AfD, Merz aliahidi kuchukua msimamo mkali kuhusu uhamiaji pamoja na kutekeleza mageuzi ya kiuchumi. Ingawa sera kali za uhamiaji zimesababisha kupungua kwa idadi ya wahamiaji wanaoingia nchini, hatua hiyo haijaongeza umaarufu wake kisiasa.

Asilimia ndogo tu ya Wajerumani ndio wanaoridhika na utendaji wa serikali ya muungano inayoongozwa na Kansela Merz Picha: Omer Messinger/Getty Images

Aidha, wachambuzi wanaonya kuwa kuipa kipaumbele ajenda ya uhamiaji kunaweza kuwa kumeimarisha zaidi vyama vya mrengo mkali. Tafiti zinaonyesha kuwa mijadala inayolenga sana uhamiaji huongeza mvuto wa vyama vya siasa kali badala ya kuupunguza.

Baadhi ya wajerumani hawaridhishwi na uongozi wa Merz

Wakati huo huo, kutoridhika kwa wananchi kunaendelea kuongezeka. Tafiti za hivi karibuni zinaonyesha kuwa ni asilimia ndogo tu ya Wajerumani wanaoridhika na utendaji wa serikali, huku wengi wakitia shaka iwapo muungano huo utaweza kudumu hadi mwisho wa muhula wake mwaka 2029.

Kutokana na hali hiyo, shinikizo linaendelea kuongezeka kwa Kansela Merz, huku baadhi ya wachambuzi wakitabiri uwezekano wa serikali yake kushindwa kumaliza muhula wake. Wakati huohuo, kupanda kwa nguvu kwa chama cha AfD kunaibua hofu mpya kuhusu mustakabali wa siasa za Ujerumani.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW