1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaRwanda

Malumbano yaendelea baina ya Kongo na Rwanda

Jean Noël Ba-Mweze
2 Desemba 2022

Kongo imemkosoa rais wa Rwanda ikisema hastahili kutoa somo la demokrasia ambayo hata haijapatikana nchini mwake,hii ni baada ya Kagame kusema Tshisekedi hakushinda uchaguzi wa 2018.

Rais wa Kongo Felix Tshisekedi na mwenzie Paul Kagame wa Rwanda
Rais wa Kongo Felix Tshisekedi na mwenzie Paul Kagame wa Rwanda

Mamlaka ya Kongo imeelezea matamshi ya Rais Paul Kagame kuwa ya kushangaza sana. Kwa hivyo Kinshasa haijaelewa jinsi rais ambaye nchi yake inakabiliwa na udikteta anaweza akaizungumzie  demokrasia.

Kinachozingatiwa na Serikali ya Kongo ni kwamba nia ya Kagame leo ni kujaribu kumyumbisha kisiasa Rais Felix Tshisekedi. Lakini kabla ya kutoa maoni yake kuhusu uchaguzi hapa Kongo, Paul Kagame anapaswa kwanza kuangalia hali nchini Rwanda, kama alivyoeleza Patrick Muyaya, Waziri wa Mawasiliano na msemaji wa serikali ya Kongo.

"Mimi nadhani kwanza Rais Kagame hastahili kutoa maoni yoyote kuhusu uchaguzi. Ni vizuri kwanza achunguze Wanyarwanda kama wana uhuru wa kujieleza,  uhuru wa kuandamana na kama yeye mwenyewe anaweza kuishi pamoja na upinzani. Nadhani kwenyi mstari wa demokrasia duniani, Rwanda ndiyo ya mwisho na hivyo si yeye ambaye anaweza kutueleza la kufanya.",alisema Muyaya.

Tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu

Raia wa Rutshuru wamekimbia mapigano baina ya jeshi na waasi wa M23Picha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Hayo yamejiri huku mapigano yakiendelea katika eneo la Rutshuru mkoani Kivu Kaskazini baina ya jeshi la Kongo na waasi wa M23 ambao Umoja wa mataifa umetambuwa wanaungwa mkono na Rwanda. Wizara ya haki za binadamu nchini Congo inawashutumu waasi hao ukiukaji  wa haki za binadamu na hivyo, Waziri wa haki za kibinadam ameahidi kufikisha kesi mbele ya mahakama ya kimataifa. Waziri Albert-Fabrice Pwela anazungumza.

"Mambo yanayotufikia ni thabiti, yameandikwa na yanathibitisha kwamba magaidi hao pamoja na jeshi la Rwanda wanawasajili watoto, wanawatumia kama ngao za binadamu na pia kuwatumia kwa kazi za kulazimishwa, huku pia wakitumia ubakaji kama silaha ya vita. Kwa hivyo, mahakama ya kimataifa sherti kushughulikia kesi hii ya ukiukwaji wa wazi wa haki za binadamu.",Pwela alisema.

Wakati hayo yote yakijiri, mazungumzo ya amani yanaendelea mjini Nairobi nchini Kenya, baina ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na makundi yanayomiliki silaha mashariki mwa nchi hii.