Malumbano yayumbisha amani Somalia
3 Desemba 2013Watalamu wa masuala ya kisiasa wameonya kuwa kutokana na mvutano kati ya viongozi hao wakuu nchini Somalia, utaiwia vigumu jumuiya ya kimataifa kufanikisha vita dhidi ya ugaidi nchini humo na kumaliza vita vya koo vilivyodumu kwa karne kadhaa.
Waziri Mkuu wa Somalia Abdi Farah Shirdon, alieingia madarakani mwaka mmoja uliopita, anakabiliana na kura ya imani bungeni wiki hii, baada ya kupingana na agizo la Rais Mohamud la kumtaka ajiuzulu.
Mpaka sasa haijafahamika vizuri nini hasa chanzo cho kutofautiana kati ya viongozi hao. Miezi sita iliyopita, Rais Mohamud alimtetea waziri mkuu wake Shirdon, wakati wabunge walipomtaka atoke madarakani. Sasa ni yeye mwenyewe ndiye anayekinzana na chaguo lake hilo na kumtaka atoke madarakani.
Chanzo cha udhaifu wa serikali ya Somalia
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Somalia wanasema huenda sababu ni tuhuma za vitendo vya rushwa serikalini, kupoteza uaminifu na hata migogoro ya kisiasa iliyopo baina ya koo, ambapo kila ukoo unataka uwakilishi katika madaraka.
Hata hivyo, kwa mujibu wa mbunge, Mohamed Yusuf, ni kwamba Shirdon amewaambia kuwa mvutano wake na Rais Mohamud unasababishwa na mambo mengi ikiwepo kutofautina katika kuchagua baraza la mawaziri.
Ubinafsi wa koo bado upo
Tatizo la kuwania madaraka nchini Somalia limechukua nafasi kubwa, katika wakati ambapo nchi hiyo ilipaswa kuimarika kiutawala na kuondoa mfumo wa kutokuwa na serikali kwa miaka mingi ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, kutokana na kila ukoo kujichukulia mamlaka ya uongozi katika eneo lake.
Serikali ya Mohamud na Shirdon iliyoingia madarakani mwezi Agosti mwaka 2012, ni ya kwanza kukubalika katika jumuiya ya kimataifa tangu nchi hiyo iliposambaratika kiutawala mwaka 1991. Jumuiya ya kimataifa imekuwa ikiapatia Somalia mabilioni a fedha kama misaada, kwa ajili ya kuijenga upya nchi hiyo upya na pia kuiwezesha kusimamia ipasavyo kupambana na ugaidi wa kundi la al-Shabaab lenye chimbuko lake nchini Somalia.
Kukithiri kwa rushwa kuiyumbisha serikali
Mapema mwezi huu, Gavana wa Benki Kuu ya nchi hiyo, Bi Yussur Abrar, alijiuzulu, akilalamikia kushurutishwa na viongozi kusaini mikataba inayofanyika kwa rushwa. Bi Yussur amekuwa wa pili kujiuzulu katika nafasi hiyo, baada ya aliyemtangulia, Abdusalam Omer, kujiuzulu katika wadhfa huo katikati ya mwezi Septemba.
Kumekuwa na shutuma zinazotolewa na maafisa wa Umoja wa Mataifa kuwa Benki Kuu ya Somalia kimekuwa chombo cha kuwanufaisha viongozi wa serikali kuu.
Kuna hofu kwamba endapo mivutano ya kisiasa ndani ya serikali itaendelea, inaweza kuanguka wakati wowote na kushindwa kama ilivyoshindwa serikali ya mpito iliyokuwepo kabla ya hii, iliyodumu kwa miaka nane.
Juu ya yote, jumuiya ya kimataifa haina budi kushirikiana na serikali dhaifu ya Somalia, kwani ni taasisi pekee ya Kisomali inayotegemewa kwa kiasi kikubwa katika mapambano dhidi ya kundi la al-Shabaab.
Serikali hiyo ilichaguliwa kwa kupewa usaidizi mkubwa na Umoja wa Mataifa mwezi Agosti mwaka jana, kwa imani kwamba ingelirejesha amani iliyopotea kwa miaka mingi ya vita vya kisiasa.
Mwandishi: Diana Kago/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef