Mambo bado Libya
23 Agosti 2011Hata katika makao makuu ya Umoja wa Afrika, AU, huko Addisababa maafisa bado wanachukuwa tahadhari. Umoja huo jana uliarifu tu kwa ufupi kwamba utakuwa na kikao kingine muhimu juu ya suala la Libya ijumaa ijayo.
Kikao maalum cha baraza la amani na usalama la Umoja wa Afrika, kilichoitishwa kwa haraka jana, hakijamua lolote, ila tu msemaji wake alisema wajumbe walibadilishana vya kutosha mawazo juu ya hali inavoendelea huko Libya. Ila tu ilikubaliwa baraza hilo likutane ijumaa ijayo, wanadiplomasia wakitaraji kwamba hadi wakati huo mambo yatakuwa wazi zaidi ili kuwawezesha wakuu wa nchi za Kiafrika kuitambua serikali mpya ya huko Tripoli.
Itakumbukwa kwamba katika nchi nyingi za Kiafrika, Muammar Gaddafi alikuwa ni mshiriki na ni mgeni anayekiaribishwa kwa mwembwe kubwa. Na serekali ya Gaddafi iliwekeza mabilioni ya fedha, kupitia miradi mbalimbali katika nchi hizo. Huko Kenya wafanya biashara wa serikali ya Gaddafi walinunua mahoteli ya fahari na nusu ya hisa katika kinu cha serikali cha kusafishia mafuta. Peke yake Libya iligharimia dola milioni 70 katika ujenzi wa bomba la mafuta linalohitajika sana kuelekea upande wa magharibi ya nchi hiyo. Na ndio maana naibu wa waziri wa mambo ya kigeni wa Kenya, Richard Onyonka, aliita siku ya jana ya ushindi wa waasi huko Libya kuwa ni siku ya huzuni kwa Afrika:
"Kama vile watu wengine, Wakenya wameona vitu vingi vizuri vilivofanywa na Gaddafi, hasa kwa vuguvugu la ukombozi katika Afrika. Ametoa mchango mkubwa katika kupambana na siasa za ubaguzi wa rangi katika Afrika Kusini na ukoloni mamboleo katika Kusini mwa Afrika. Pale wapiganiaji huru walipotaka kuungwa mkono, Gaddafi alisaidia."
Na mambo yakiwa sio wazi kabisa katika mji mkuu wa Tripoli, Rais wa Marekani, Barack Obama, jana alionya juu ya vitendo vya ulipaji visasi na utumiaji wa mabavu katika Libya.
" Haki za Walibya wote lazima ziheshimiwe. Haki ya kweli haiji kupitia vitendo vya ulipaji visasi, lakini kupitia masikilizano, na Libya inayoruhusu raia wake kuamuwa mustakbali wao."
Kuhusu hali ilivobadilika huko Libya, katibu mkuu wa Umoja wa Matafa, Ban Ki-Moon alitoa mwito ufuatao:
"Nayatolea mwito majeshi ya Gaddafi kuacha vita mara moja na kutoa nafasi ya kipindi cha mpito kwa ajili ya utulivu. Nimepanga kufanya mkutano wa dharura wiki hii na viongozi wa nchi za eneo hilo na wa kimataifa, ukiwemo Umoja wa Afrika, Umoja wa Nchi za Kiarabu- Arab League- jumuiya ya nchi za Kiislamu na Umoja wa Ulaya."
Mjini Paris, maafisa wa serikali ya nchi hiyo wameonya kwamba ushindi dhidi ya Muammar Gaddafi bado sio kamili. Waziri wa mambo ya kigeni wa nchi hiyo, Alain Juppe, alisema ushindi sio kamili, kweli ni mwisho wa udikteta, na lengo linafikiwa. Na waziri wa ulinzi wa nchi hiyo, Gerard Longuet, ambaye alisema jana kwamba utawala wa Gaddafi umeshaanguka, na kwamba mabadiliko ni kamili, baadae alisema katika radio ya nchi hiyo kwamba huko Libya hali ya mambo haijamalizika kabisa, mbali na hivyo.
Na waziri wa mambo ya kigeni wa Italy, Franco Frattini, alisema nchi yake inataraji kandarasi zilizopewa makampuni ya Italy katika Libya zitaheshimiwa na serikali mpya itakayochukuwa madaraka ikiwa waasi watamuangusha kutoka madarakani Muammar Gaddafi. Italy imepewa kandarasi zenye thamani ya mabilioni ya dola katika sekta za ulinzi na ujenzi.
Na afisa mmoja wa Israel alisema nchi yake inataraji majeshi ya waasi huko Libya yatapata ushindi kamili. Alisema Gaddafi alikuwa ni kichekeso, mara fulani alikuwa mpumbavu, lakini ni mtu wa hatari, kwa vile alijihusisha na ugaidi.
Pia Iran iliwapongeza wananchi wa Libya baada ya waasi kuingia Tripoli. Shirika rasmi la habari la nchi hiyo, IRNA, liliinukuu taarifa ya wizara ya mambo ya kigeni ya nchi hiyo ikisema kwamba uasi wa wananchi katika Libya umeonesha kwamba kuyakubali matakwa halali ya wananchi na kuheshimu mawazo yao ni jambo la lazima lisilokatalika.
Mwandishi: Othman, Miraji/Engelhardt, Marc/ZR
Mhariri: Mohammed Abdulrahman