1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mambo matano ya kuzingatiwa katika mkutano wa kilele wa G7

26 Mei 2017

Mkutano wa kilele wa viongozi wa mataifa 7 yaliyoendelea duniani waanza hii leo katika mji wa Taormina nchini Italia. Viongozi wa kundi hilo la G7 watarajiwa kuungana pamoja katika mapambano dhidi ya ugaidi

Italien G7 Treffen der Energieminister in Rom Carlo Calenda
Picha: picture-alliance/AA/R. De Luca

Viongozi wa Marekani, Kanada, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Japan na mwenyeji Italia wanahudhuria mkutano huo wa kilele wa mataifa 7 yaliyoendelea kiviwanda duniani ambapo wanatarajiwa kushughulikia masuala ya sera za kigeni na usalama miongoni mwa masuala mengine katika mkutano wao wa siku mbili lakini mambo matano yanapaswa kufuatiliwa kwa ukaribu.

Kwanza: Mkutano huo unahudhuriwa na marais wawili wapya, rais wa Marekani Donald Trump na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.  Wote wawili ni wanagenzi katika maswala ya kimataifa kwa hivyo mkutano huo wa mjini Sicily utakuwa ni fursa kwa marais hao ya kuweza kufahamiana na viongozi wengine.  Macho yote hata hivyo yatamgeukia Trump ambaye amekuwa akitoa ishara tofauti tofauti katika masuala ya ulimwengu kama vile uhusiano wake na Urusi na Iran, kitisho cha nyuklia kutoka Korea Kaskazini na mzozo wa Syria. Vilevile tunashuhudia jambo lisilo la kawaida katika kundi hili la G7 ambapo viongozi wengine wanapoingia wengine wanajiandaa kuondoka kwani mkutano huo wa kilele wa Taormina unaweza ukawa ndio wa mwisho kwa waziri mkuu wa Uingereza Theresa May, mwenziwe wa Italia Paolo Gentiloni na labda pia kwa kansela wa Ujerumani Angela Merkel.

Mawaziri wa nishati wa nchi wanachama wa G7Picha: picture-alliance/AA/R. De Luca

Pili: hadi kufikia mwaka jana jamii ya kimataifa ilikuwa inazungumza lugha moja ukizingatia kupunguza kiwango cha joto duniani na kutafuta njia kwa pamoja za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi. Lakini kwa sasa mustakabali huo unayumbayumba kutokana na rais wa Marekani Donald Trump anayependelea sera yake ya biashara ya 'Marekani Kwanza' huku akiwa anapuuzilia mbali maswala yanayohusiana na mabadiliko ya hali ya hewa akiyafananisha na mzaha tu. Trump amesema atatoa maamuzi yake juu ya mkataba wa Paris wa makubaliano kuhusu mabadiliko ya tabia nchi baada ya mkutano wa Taormina kumalizika. Ujerumani na Ufaransa huenda ndio zikawa nchi zitakazo ikabili Marekani kutokana na msimamo wake lakini Italia ambayo ndiye mwenyeji, wanadiplomasia wake wanang'ang'ana kuweka mambo sawa baada ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa G7 uliofanyika mwezi Aprili kushindwa kufikia makubaliano kutokana na ugeugeu wa Marekani katika masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa.  Mshauri wa rais Trump katika masuala ya uchumi Gary Cohn amesema kwa Marekani kukubaliana na mkataba wa Paris kuhusu mabadiliko ya tabia nchi itakuwa ni sawa na kuudumaza ukuaji wa uchumi wa nchi hiyo.

Waziri mkuu wa Italia Paolo Gentiloni na rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Reuters/K. Lamarque

Tatu: Italia vilevile inawataka wanachama wa G7 wawajibike katika kuleta utulivu nchini Libya ambako wahamiaji wengi wanatokea kuingia nchini humo. Pia suala jingine ni kuhusu mpango wa maendeleo kwa bara la Afrika. Tunisia, Nigeria, Kenya, Ethiopia, Umoja wa Afrika na benki ya maendeleo ya Afrika zimealikwa kujadili suala hilo. Kuna hofu huenda Marekani na Uingereza zikapinga iwapo majadiliano juu ya uhamiaji yatavuka na kuingia katika masuala ya kulinda mipaka. 

Nne: Kundi hilo la mataifa 7 yaliyoendelea duniani hapo zamani lilikuwa kundi la mataifa manane kabla ya Urusi kufukuzwa kutokana na hatua yake ya mwaka 2014 ya kuikata Crimea kutoka Ukraine, na wala hakuna dalili kama Urusi itarejeshwa hivi karibuni lakini suala la kuishirikisha nchi hiyo bado linabakia kuwa mwiba wa kooni kwa baadhi ya wanachama wa G7 kwa sababu Urusi ni kiungo muhimu katika masuala mbalimbali ya ulimwengu.  Masuala hayo ni pamoja na Libya, Syria na Korea Kaskazini. Mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa G7 wa mwezi Aprili ulipinga pendekezo la Uingereza ilipotaka Urusi iwekewe vikwazo zaidi kwa sababu ya kumuunga mkono mshirika wake rais Bashar al Assad wa Syria.

Na Tano:  Hoja zingine ni ahadi zinazohusiana na dunia utandawazi na maendeleo kwa jumla. Italia inataka ahadi za G7 zitimizwe hasa katika kubana mianya ya kodi inayotumiwa na makampuni ya kimataifa. Italia pia inataka wanawake wapewe uwezo zaidi.

Mwandishi: Zainab Aziz/DPAE/APE/RTRE

Mhariri: Iddi Ssessanga