Mambo yanazidi kuwa moto Syria
6 Julai 2011Si chini ya watu 22 wameuliwa katika msako mkali uliofanywa na majeshi ya usalama ya Syria katika mji usiokuwa tulivu wa Hama, katikati ya nchi hiyo. Wanaharakati wamesema hayo leo, huku upinzani ukikataa kushiriki katika mdahalo wa kitaifa ambao umeandaliwa na serekali ya nchi hiyo.
Jumuiya ya kitaifa ya Syria juu ya haki za binadamu imesema katika taarifa, nakala yake imepatikana na shirika la habari la Ujerumani, dpa, kwamba zaidi ya watu 50 wamejeruhiwa, wengine vibaya, katika msako huo uliofanywa Hama. Ilisema majeshi ya usalama yalivamia hospitali ya Al Hurani katika mji huo ambao ulishuhudia ijumaa iliopita maandamano makubwa dhidi ya utawala wa Rais Bashar al-Assad. Ripoti kama hizo ni taabu kuzihakikisha kwa vile serekali ya Syria inayakataza mashirika ya habari ya kigeni kuingia katika nchi hiyo.
Lakini serekali ya Syria inavilaumu vikundi vinavoipinga kwamba jana viliweka vizuizi majiani na kuchoma matairi ya magari katika maeneo kadhaa ya Hama. Shirika la habari la Syria lilisema kwamba majeshi ya usalama yalijiingiza kurejesha usalama na utulivu katika maeneo hayo, ambako yalishambuliwa na vikundi venye silaha. Vikundi hivyo viliwasha moto na kutumia mabomu ya misumari. Kikundi cha upinzani kilisema leo kwamba kitasusia mkutano wa mdahalo wa kitaifa ulioitishwa na Rais al-Assad na makundi mengi yatachukuwa hatua kama hiyo, yakisema hayatahudhuria mazungumzo ya mwezi July kwa vile ajenda ya mkutano huo haitambuwi kiini cha mzozo wa sasa nchini humo, ambao, kwa mujibu wa fikra zao, ni kudharauliwa haki halali za raia
Mazungumzo hayo yaliitishwa na Rais al-Assad pale alipotoa hotuba mwishoni mwa mwezi Juni kama sehemu ya marekebisho ya kisiasa yalioahidiwa, ikiwa ni pamoja na kuibadilisha katiba kwa lengo la kukomesha maandamano dhidi ya utawala wake uliodumu sasa miaka 11. Mwanachama wa kikundi cha upinzani, Luai Husseini, amesema watakaoshiriki katika mdahalo unaokuja hawana haki ya kutunga katiba mpya kabla ya mlango kuwekwa wazi kwa ajili ya uhuru wa wananchi nchini Syria.
Katika ripoti iliotolewa ljana, shirika la kupigania haki za binadamu duniani, Amnesty International, lilitaja kile ilichokitaja kuwa ni uhalifu dhidi ya ubinadamu unaofanywa na majeshi ya usalama ya Syria katika kuwakandamiza wanaharakti wa demokrasia. Shirika hilo limelihimiza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulizusha suala la vitendo vya majeshi ya usalama ya Syria mbele ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa vita, kuiwekea vikwazo vya silaha nchi hiyo na kuzizuwia mali za Rais al-Assad na wasaidizi wake.
Mwandishi: Miraji Othman/ dpa/afp
Mhariri. Mohammed Abdulrahman