Mambo yatokota Syria, 50 wauwawa Homs
6 Februari 2012Mji wa Homs umekuwa kitovu cha mapambano baina ya vikosi vya serikali na makundi yaliyojihami ambayo yanaupinga utawala wa rais Bashar al Assad. Mkuu wa Baraza la Kitaifa la Syria ambalo ni kundi la upinzani nchini humo, Catherine al-Talli, amesema idadi ya vifo walivopokea tangu kuanza kwa mashambulizi hayo saa kumi na mbili asubuhi ya leo imefika 50, huku wengi waliouwawa wakiwa raia.
Mashambulizi hayo yanakuja siku moja baada ya Marekani, kuahidi vikwazo vikali zaidi dhidi ya Syria, katika kuijibu hatua ya Urusi na China kutumia kura zao za turufu, kuupinga mswaada wa azimio la Umoja wa Mataifa ambao ungeunga mkono mpango wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu unaomtaka Rais Assad aondoke madarakani.
Marekani kusimama na Wasyria
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton, alisema Marekani itasimama kidete pamoja na raia wa Syria wanaotaka demokrasia. Bibi Clinton alisema Marekani itashirikiana na mataifa mengine, ili kujaribu kuwatambua wale ambao wanaufadhili utawala wa Assad, na kuutumia silaha ambazo zinatumika kuwaangamiza Wasyria wasioweza kujilinda, wakiwemo wanawake na watoto.
Wakati huo huo, ndani ya Syria kwenyewe kumesikika mripuko ulioliharibu bomba la mafuta la kiwanda kikuu cha mji wa Homs na moshi mkubwa umeonekana katika eneo hilo. Wakaazi pamoja na watu walioshuhudia wamesema mripuko huo, ambao ni wa pili katika wiki moja kulilenga bomba hilo ambalo husafirisha mafuta ghafi kutoka kisima cha mafuta cha Rumailan, ulitokea katika wilaya ya Bab Amro. Mabomba kadhaa ya mafuta yameharibiwa mkoani humo kutokana na miripuko katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita.
Urusi na China zajitetea
Kwingineko, Waziri wa Mambo ya kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov, amesema kuidhinishwa kwa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo lilitungwa na Mataifa ya Magharibi na Kiarabu, kungemaanisha kuegemea upande mmoja katika kuzua vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Akiutetea uamuzi wa Urusi kupinga azimio hilo kwa kutumia kura ya turufu, Lavrov alisema rasimu hiyo ilitoa masharti kwa upande wa serikali na vikosi vyake, lakini pia ilipaswa kujumuisha kwa kiwango fulani makundi ya upinzani yanayoibua ghasia.
China pia imeitetea hatua yake ya kuukataa mswada wa azimio la Umoja wa Mataifa uliomtaka Assad ajiondoe madarakani, huku vyombo vya habari vya serikali vikisema hatua ya mataifa ya Magharibi kuingilia Libya, Afghanistan na Iraq ilionyesha dosari katika kulazimisha mabadiliko ya utawala.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya nje, Liu Weimin, amesema China kila mara inayachukulia kwa umuhimu mkubwa matukio yanayoendelea nchini Syria, na wakati wote imezitaka pande zote mbili nchini humo zisitishe ghasia na hasa kuepuka vifo miongoni mwa raia. Aliongeza kuwa China haiungi mkono upande wowote nchini Syria unaoshiriki katika mashambulizi.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters
Mhariri:Miraji Othman