Mamia waachiwa huru na IS Syria
14 Agosti 2016Katika eneo jingine, raia kadhaa waliuwawa jana Jumamosi katika shambulio la ndege za kijeshi za jeshi la serikali ya Syria pamoja na washirika wao wa Urusi, na katika mashambulizi ya makombora yaliyofanywa na waasi katika eneo la mapigano katika jimbo la Aleppo, limesema kundi linaloangalia hali nchini humo.
Kiasi ya raia 51 ikiwa ni pamoja na watoto waliuwawa mjini Aleppo na linalozunguka mji huo, wakati raia wengine 22 waliuwawa katika jimbo jirani la Idlib, shirika linaloangalia haki za binadamu nchini Syria limesema.
Wapiganaji wa mwisho wa kundi la IS walikimbia kutoka mji wa Manbij karibu na mpaka na Uturuki siku ya Ijumaa baada ya kushambuliwa na wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon kusema inaonekana kuwa wapiganaji hao wenye itikadi kali wamekabwa.
Kukimbia kutoka mji huo ambao ulikamatwa na wapiganaji wa IS mwaka 2014 ilikuwa pigo kubwa kabisa kwa wapiganaji hao wa jihadi kuwahi kutokea dhidi ya vikosi vya Syrian Democratic Forces SDF, muungano wa Wakurdi na Waarabu unaoungwa mkono na mashambulizi ya anga ya Marekani.
Ngao ya binadamu
Wapiganaji wanaokimbia waliondoka pamoja na kiasi ya raia 2,000, ikiwa ni pamoja na wanawake na watoto, siku ya Ijumaa kuzuwia mashambulizi ya anga wakati wakielekea katika mji wa mpakani unaoshikiliwa bado na kundi hilo wa Jarabulus, kwa mujibu wa wapiganaji hao wa SDF.
Kiasi ya baadhi ya watu waliochukuliwa na wanamgambo hao baadaye waliachiliwa ama walitoroka, vikosi hivyo vya muungano vilisema jana Jumamosi, lakini haijulikani watu wengine wako wapi.
"Hakuna wapiganaji tena wa IS" waliobakia mjini Manbij, mpiganaji mmoja wa SDF alisema.
Televisheni ya Wakurdi ilionesha picha za raia wakifurahia mjini Manbij, ikiwa ni pamoja na akina mama waliokuwa wakitabasamu, ambao waliondoa hijabu zao na wanawake waliwakumbatia wapiganaji wa Kikurdi.
Mwanamke mmoja alichoma nguo nyeusi ambayo wapiganaji hao wa jihadi waliwalazimisha wakaazi kuvaa, wakati wanaume ambao waliishi kwa wiki kadhaa wakilazimishwa kuacha ndevu zao bila kuzinyoa , walizinyoa.
Mabomu kila nyumba
"Mapambano yalikuwa makali," duru kutoka kwa wakurdi zimezungumza na shirika la habari la afp, na kuongeza wapiganaji wa jihadi waliweka mabomu katika mji huo.
"Mmoja kati ya wapiganaji wa SDF aliingia katika nyumba siku ya Ijumaa na kuona kiatu kimewekwa juu ya kitabu cha Koran. Alipokiondoa kulikuwa na mripuko na aliuwawa," duru hiyo ilisema.
Mkaazi mmoja aliliambia shirika la habari la afp hakukuwa na hata nyumba moja katika eneo anakoishi ambalo halikutegwa mabomu.
"Tunawaomba watu wanaohusika kuchukua hatua" ya kuyaondoa mabomu hayo, Jamal Abul Ababiyya alisema, na kuongeza kwamba mabomu yanawajeruhi watu kila siku.
Picha za shirika la habari la afp zinaonesha mitaa ya mji huo ikiwa imetapakaa taka na ukuta bado ukiwa umechorwa bendera ya wapiganaji hao wa jihadi yenye rangi nyeusi na nyeupe.
Mwandishi: Sekione Kitojo/afp
Mhariri: Josephat Charo