Mamia waandamana wakati Senegal ikisubiri tarehe ya uchaguzi
25 Februari 2024Mamia ya raia wa Senegal waliandamana katika mji mkuu wa Dakar Jumamosi, kumuunga mkono na wengine wakimpinga Rais Macky Sall. Maandamano hayo yamefanyika wakati taifa hilo likiwa katikati ya mgogoro wa kisiasa uliotokana na kucheleweshwa uchaguzi wa Rais uliokuwa umepangwa kufanyika leo Jumapili.
Maandamano ya kumpinga rais yametokana na wito uliotolewa na muungano wa vyama vya kisiasa na asasi za kiraia wa F24 unaotaka uchaguzi ufanyike.
Nao waandamanaji wanaomuunga mkono Rais Sall walikusanyika katika eneo la makaazi ya watu mjini Dakar wakiwa wamebeba bendera za Senegal wakitetea rekodi yake na kusema kuwa amefanya megi.
Rais huyo wa Senegal amekumbana na upinzani mkali tangu alipotangaza kuuchelewesha uchaguzi wa rais wa Februari 25. Hata hivyo Baraza la Katiba la nchi hiyo liliupindua uamuzi huo na kutaka uitishwe haraka iwezekanavyo.