1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mamia waandamana Davos kupinga uroho wa mataifa tajiri

16 Januari 2023

Viongozi na wafanyabiashara wakubwa duniani wameanza kuwasili Davos kwa ajili ya mkutano wa uchumi duniani, huku wakilakiwa na maandamano ya wanaharakati wanaopinga unyonyaji wa mataifa tajiri dhidi ya mataifa masikini.

WWF Davos 2023 Auftakt/Protest
Picha: Arnd Wiegmann/REUTERS

Mamia ya waandamanaji walijitokeza katika mji wa milimani wa Davos kuwalaki viongozi na wafanyabiashara wakubwa waliokuwa wakiwasili kwa mabango ya kupinga kile walichokiita "dhuluma na unyonyaji wa matajiri dhidi ya masikini ulimwenguni."

Kampuni za mafuta na chakula zilitajwa na wanaharakati hao kuwa zimetumia mizozo inayopamba moto sasa ulimwenguni kujifaidisha kifedha. 

Shirika la kupambana na umasikini duniani, Oxfam International, lilitaka kampuni za chakula zitozwe kiwango cha juu cha kodi ili kupunguza hali ya ukosefu wa usawa ulimwenguni.

Mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo, Gabriela Bucher, amesema asilimia moja tu ya watu duniani inawazidi asilimia 99 ya wenzao kwa utajiri:

Soma zaidi: Matajiri waomba kutozwa kodi
                    Oxfam: Mabilionea watajirika maradufu wakati wa Covid-19

"Ripoti yetu iitwayo 'Mwenye Nguvu Mpishe' inaonesha kwamba asilimia moja ambao ndio matajiri kabisa wanakokozowa thuluthi mbili ya utajiri mpya tangu mwaka 2022. Hiyo ni sawa na mara mbili ya walichonacho wanaadamu asilimia 99 waliobakia panapohusika utajiri wao kwenye kipindi hiki. Na inaipiku hali ilivyokuwa miaka kumi iliyopita, ambapo wakati huo asilimia hiyo moja ya matajiri walikuwa wanajikusanyia nusu ya utajiri wote wa dunia." Alisema mkurugenzi huyo.

Viongozi wa mataifa tajiri wakwepa

Ripoti hiyo ya Oxfam iliyotolewa siku ya Jumatatu (Januari 16) leo kwa lengo la kuchochea mjadala kwenye vikao vya wanasiasa na wafanyabiashara kwenye mkutano huu wa uchumi duniani, ilisema dunia imejikuta ikikabiliwa na mizozo mingi kwa wakati mmoja na yote inachochea kuongezeka kwa umasikini.

Baadhi ya waandamaaji wanaopinga uroho wa mataifa tajiri ulimwenguni wakiwa kwenye maandamano ya Davos.Picha: Arnd Wiegmann/REUTERS

Mizozo hiyo ni mabadiliko ya tabianchi, kupanda kwa gharama za maisha, uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na janga la UVIKO-19, ambayo licha ya kuongeza ufukara kwa walio masikini, "matajiri wamezidi kuwa matajiri na faida kwa kampuni kubwa zimepanda kwa kasi ya ajabu."

Soma zaidi:Oxfam yasema tofauti ya kipato kati ya matajiri na masikini ni kubwa sana

Mkutano wa mwaka huu wa uchumi duniani unawakutanisha viongozi kutoka zaidi ya mataifa 50 duniani, lakini tayari kulikuwa na taarifa za viongozi wa mataifa tajiri zaidi kuukwepa na badala yake kutuma wawakilishi wao.

Miongoni mwa mataifa saba yaliyoendelea kwa uchumi wa viwanda, ni Ujerumani pekee iliyowakilishwa na kiongozi wake mkuu wa serikali ya shirikisho, Kansela Olaf Scholz. 

Hata Afrika Kusini, moja ya mataifa yanayoinukia kiuchumi kupitia jumuiya ya BRICS, haitawakilishwa tena na Rais Cyril Ramaphosa, ambaye amelazimika kuahirisha safari yake kushughulikia tatizo kubwa la umeme nchini mwake.

Ramaphosa alitazamiwa kushirikiana na Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania kuongoza ujumbe wa Afrika kwenye kongamano hilo kubwa kabisa la uchumi duniani. 
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW