Mamia waandamana Kenya kupinga matumizi makubwa ya plastiki
11 Novemba 2023Maandamano hayo yamefanyaka kuelekea mkutano utakaojadili njia za kushughulikia kile kinachotajwa kuwa "kizaazaa cha matumizi ya plastiki" ulimwenguni.
Wawakilishi kutoka zaidi ya mataifa 170 watakusanyika mjini Nairobi kuanzia siku ya Jumatatu kwa majadiliano juu ya hatua nzito zinazopaswa kuchukuliwa ikiwemo kupata mkataba ulio na nguvu kisheria utaofikisha mwisho uchafuzi wa mazingira unaotokana na matumizi ya plastiki.
Waandamanaji walijikusanya leo walibeba mabango yenye ujumbe unaosomekana "janga la plastiki ni sawa sawa na mzozo wa mabadiliko ya tabianchi" na mengine ya kutoa mwito wa kuvilinda vizazi vijavyo dhidi ya taathira za plastiki.
Uzalishaji wa bidhaa za plastiki duniani umeongezeka maradufu tangu mwanzoni mwa karne ya 21 na kufikia tani milioni 460 kwa mwaka hali inayoongeza kitisho kwa mazingira hususani kwa viumbe vya baharini.