Mamia waandamana kupinga uchimbaji haramu wa madini Kongo
8 Januari 2025Matangazo
Mamia ya watu wameandamana katika jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, kupinga uchimbaji haramu wa madini,mashariki mwa nchi hiyo,ambako maafisa wanachunguza madai ya kusambaa kwa visa vya kuhusika kwa raia wa China kwenye shughuli hizo haramu.
Maandamano hayo yamefuatia tangazo la Jumapili la kukamatwa kwa raia watatu wa China waliokutwa na dhahabu pamoja na pesa nyingi taslimu, kwa mujibu wa gavana wa Kivu Kusini Jean Jacques Purusi.
Maafisa wa mkoa huo Mashariki mwa Kongo wenye utajiri wa madini wanasema mamia ya makampuni ya uchimbaji madini na hasa ya Wachina, yanachimba dhahabu bila ya kuonesha faida wanazopata kwa vyombo husika na mara nyingi shughuli hizo hufanywa bila ya vibali halali.