1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiMorocco

Mamia wafa katika tetemeko la ardhi Morocco

Sylvia Mwehozi
9 Septemba 2023

Takribani watu 300 wamekufa baada ya tetemeko kubwa la ardhi kupiga nchini Morocco usiku wa kuamkia leo na kuharibu majengo katika mji wa Marrakesh.

Marocco- Casablanca
Raia wakiwa wamekusanyika mitaani huko Casablanca Picha: Abdelhak Balhaki/REUTERS

Wakaazi katika miji kadhaa muhimu ya Morocco ikiwemo mji wa kihistoria wa Marrakesh wametikiswa na tetemeko kubwa la ardhi usiku wa kuamkia Jumamosi.

Wizara ya mambo ya ndani imesema katika taarifa yake kwamba "kulingana na ripoti za awali, tetemeko la ardhi limewaua watu 296 katika majimbo ya na manispaa za Al-Haouz, Marrakesh, Ouarzazate, Azilal, Chichaoua na Taroudant". Watu wengine 153 wamejeruhiwa kulingana na ripoti za serikali.Tetemeko la ardhi Uturuki na Syria laangamiza watu 24,000

Raia katika mji ulioathirika zaidi wa Marrakesh, wamesema kuwa baadhi ya majengo yameporomoka katika mjio huo wa kale na wa kihistoria huku video za kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha majengo yaliyogeuka kuwa vifusi na vumbi. Kitovu cha tetemeko hilo kilikuwa juu katika Milima ya Atlas takriban kilomita 70 kusini mwa mji wa Marrakesh. Vyombo vya habari vya Morocco vimelitaja kuwa tetemeko lenye nguvu zaidi kuwahi kuikumba nchi hiyo.

Athari za tetemeko la ardhi MoroccoPicha: Al Oula TV via REUTERS

Mamlaka ya Morocco inayofuatilia matetemeko ya ardhi imelitaja kuwa katika ukubwa wa 7.2 katika kipimo cha Richter wakati mamlaka ya Jiolojia ya Marekani ikisema tetemeko hilo lilikuwa na ukubwa wa 6.8.

Mkaazi wa kijiji cha mlimani cha Asni karibu na chanzo cha tetemeko hilo Montasir Itri, amesema kwamba nyumba nyingi zimeharibiwa. "Majirani zetu wako chini ya vifusi na watu wanafanya kazi kwa bidii kuwaokoa kwa kutumia njia zilizopo kijijini.”

Tetemeko hilo pia lilisikika katika miji ya pwani ya Rabat, Casablanca na Essaouira na katika nchi jirani ya Algeria.Tetemeko la ardhi Uturuki-Syria

Mnamo mwaka wa 2004, takriban watu 628 walifariki na 926 walijeruhiwa wakati tetemeko la ardhi lilipopiga Al Hoceima kaskazini mashariki mwa Morocco. Tetemeko la ardhi la El Asnam la mwaka 1980 katika nchi jirani ya Algeria lilikuwa mojawapo ya matetemeko makubwa na ya uharibifu zaidi katika historia ya hivi karibuni. Liliwaua watu 2,500 na kuacha angalau 300,000 bila makaazi.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW