1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mamia wafa kwa mafuriko Pakistan, Afghanistan

5 Agosti 2013

Mvua kubwa katika mataifa ya Afghanistan na Pakistan imeua zaidi ya watu 160 , huku maelfu ya wanavijiji wakiachwa bila makaazi, chakula wala umeme katika janga kubwa kabisa la kimaumbile kuwahi kushuhudiwa mwaka huu.

epa03812863 People evacuate flooded areas after heavy downpour in the country's largest city, Karachi, Pakistan, 04 August 2013. At least 70 people were killed in different parts of the country following heavy monsoon rains. EPA/REHAN KHAN
Überschwemmung Pakistan KarachiPicha: picture-alliance/dpa

Maeneo ya milimani ndiyo yaliyoathirika vibaya zaidi, ambako watu 61 wamepoteza maisha na kiasi cha nyumba 500 za udongo zimesombwa na maji katika vijiji kadhaa wilaya ya Sarobi, iliyo umbali wa mwendo wa saa moja kutokea mji mkuu, Kabul.

Kwa mujibu wa maafisa wa serikali, jimbo la mashariki la Nuristan limeshuhudia nyumba 60 zikiharibiwa kabisa na mafuriko hayo, ingawa hakuna mtu aliyeripotiwa kupoteza maisha.

Msemaji wa jimbo hilo, Mohammad Yusufi, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba wameomba msaada wa serikali kuu, lakini hilo ni eneo linaloendeshwa na wapiganaji wa Taliban.

Kiasi cha watu wengine 24 wamefariki dunia katika majimbo mengine mawili yaliyo mpakani na Pakistan - Khost na Nangahar. Huko nako zaidi ya nyumba 50 na maduka yamesombwa na maji huku maelfu ya ekari za mashamba zikighariki.

Pakistan yakumbwa tena

Nchini Pakistan, mvua hizi za masika zimegharimu maisha ya watu 80, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya huko. Matukio ya nyumba kuporomoka, kuzama kwenye maji na shoti za umeme, ndiyo yaliyopelekea idadi hiyo ya vifo, amesema Waziri wa Habari wa Pakistan, Sharjeel Inam Memon.

Watu wakikimbia mafuriko kwenye vijiji vya Pakistan.Picha: picture-alliance/dpa

Hata mji mkuu wa kibiashara na wa bandari ya kusini, Karachi, haukusalimika. Viunga vya watu masikini kwenye mji huo wenye wakaazi milioni 18 vinaelea kwenye maji, na nyumba kadhaa hazina huduma ya umeme. Vifo vimeripotiwa pia kwenye maeneo ya kaskazini na magharibi ya nchi hiyo.

Mvua hiyo ya siku tatu inatajwa kuwa janga kubwa kabisa kuwahi kutokea kwenye eneo hilo katika siku za karibuni. Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Pakistan imeonya hivi leo kwamba bado kutakuwa pepo kali na mvua nyingi inatarajiwa kunyesaha, ambapo mito itaendelea kufurika.

Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Nawaz Sharif, amewatuma mawaziri wake watatu kwenda kwenye maeneo yaliyoathirika vibaya zaidi. Ndani ya kipindi cha miaka hii mitatu, Pakistan imekuwa ikikumbwa na mafuriko takribani kila mwaka.

Mabaya zaidi yalikuwa ya mwaka 2010, ambapo watu 1,800 walipoteza maisha na milioni 21 kuathiriwa na mvua kali za msimu wa masika.

Wataalamu wa hali ya hewa duniani, wanalaumu mabadiliko ya tabia nchi kuwa ndio chanzo cha majanga haya makubwa ya kimaumbile.

Maeneo yaliyo kwenye ukanda wa Bahari ya Hindi yanatajwa kuwa kwenye wasiwasi, ingawa hadi sasa hakujatangazwa kitisho cha wazi na cha moja kwa moja.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP/AP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW