Mamia wakamatwa katika maandamano Tunisia
12 Januari 2018Tunisia, ambayo mapinduzi ya mwaka 2011 yalichochea vuguvugu la mabadiliko katika nchi za kiarabu, imekumbwa na maandamano yenye vurugu tangu Jumatatu, ambayo yameshuhudia waandamanaji wakipambana na vikosi vya usalama na kuwaacha watu kadhaa wakijeruhiwa.
Taifa hilo la Afrika ya Kaskazini linaonekana kuwa hadithi yenye mafanikio kidogo ya vuguvugu la mapinduzi ya miaka saba iliyopita ambayo yaliondoa utawala wa siku nyingi katika ukanda huo, lakini kushindwa kwake kushughulikia umaskini na ukosefu wa ajira kumechangia chuki ya kiuchumi.
Katika vurugu za hivi karibuni, vijana kwenye mji wa kaskazini wa Siliana, waliwapiga maafisa wa usalama kwa mawe na mabomu ya mikono, ambao waliwajibu kwa kutumia gesi za kutoa machozi, kwa mujibu wa shirika la habari la AFP.
Wizara ya mambo ya ndani imesema polisi waliwakamata watu 328 siku ya Jumatano kwa wizi pamoja na kuzuia barabara, ikiwa ni nyongeza ya watu 280 waliokamatwa siku mbili zilizopita. Msemaji wa wizara Khalifa Chibani amesema vurugu hizo hazikuwa kubwa ukilinganisha na zile za siku za nyuma.
Maafisa 21 wa usalama walijeruhiwa, kwa mujibu wa Chibani na kuongeza kwamba hakuna raia aliyejeruhiwa. Mwandishi wa AFP wa eneo hilo alisema maeneo mengi yalikuwa na utulivu siku ya Alhamis jioni na rais amesema atakutana na vyama vikuu, vyama vya wafanyakazi na vile vya wafanyabiashara siku ya jumamosi kujadili juu ya hali hiyo. Tunisia ilionekana kuwa na kipindi kizuri cha mpito tangu yalipotokea mapinduzi yaliyomuondoa dikteta wa siku nyingi Zine El Abidine Ben Ali.
Lakini Watunisia wenyewe wameelezea kuchanganyikiwa tangu kuanza kwa mwaka na hatua za kukabiliana na hali mbaya uchumi zinazotarajiwa kuongeza zaidi bei katika uchumi unaosua sua.
Nchi hiyo imeanzisha ongezeko la kodi ya thamani na michango ya kijamii kama sehemu ya bajeti mpya. Wanaharakati wanaopinga hatua hizo wameitisha maandamano makubwa siku ya Ijumaa.
Vurugu zilianza na maandamano ya amani wiki iliyopita lakini yalisambaa na kugeuka kuwa mapambano na polisi usiku wa Juamatatu na Jumanne. Vurugu pia ziliyakumba maeneo kadhaa kati kati mwa miji ya Kasserine na Siliana, Tebourba na Thala huko kaskazini. Mapambano pia yaliibuka katika baadhi ya vitongoji vya Tunis. Siku ya Alhamis, watu kadhaa wasio na ajira waliandamana kati kati mwa mji wa Sidi Bouzid, kitovu cha maandamano yaliyochochea vuguvugu la 2011.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP
Mhariri: Saumu Yusuf