Mamia wapinga kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Sudan
25 Oktoba 2021Katika taarifa iliyotolewa na Wizara ya habari katika ukurasa wa Facebook, wanachama wa kiraia katika baraza linalotawala Sudan na mawaziri katika serikali ya mpito ya waziri mkuu Abdalla Hamdok, nao pia wamekamatwa. Huduma za inteneti zimekatwa kote nchini huku barabara kuu na madaraja yanayounganisha mji mkuu wa Khartoum vikifungwa.
Wanajeshi walivamia makao makuu ya Televisheni ya taifa ya Sudan iliyoko katika mji wa Omdurman, wakati nyimbo za kizalendo zikirushwa katika televisheni. Watu wameingia mitaani, wakichoma matairi na kupanga matofari barabarani wakipinga hatua ya jeshi. Taarifa zaidi zinasema kwamba Waziri mkuu Hamdok na mawaziri wake wamepelekwa eneo lisilojulikana.
Mmoja wa waandamanaji amepinga hatua ya jeshi. "Huu ni wito wa dharura kwa raia wote wa Sudan ambao wanataka kulinda mapinduzi yao, kinachofanywa na jeshi ni usaliti kwa raia wote katika pande zote. Ni wajibu wa raia wote kupinga na kuzuia barabara zote za nje, kuzuia vikosi vyovyote vya jeshi kusonga. Hivi sasa sote tunapaswa kuungana kuonyesha ukweli."
Mjumbe maalumu wa Marekani katika pembe ya Afrika Jeffrey Feltman amesema Washington "ina wasiwasi mkubwa na ripoti za jeshi kuchukua mamlaka ya serikali ya mpito". Umoja wa Mataifa nao umeelezea kukamatwa kwa viongozi hao kuwa hatua "isiyokubalika".
Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya nchi za Kiarabu nazo zimeleezea wasiwasi zikitaka wadau wote na washirika wa kikanda kurejesha serikali ya mpito. Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas ametoa wito "kwa kila mtu nchini Sudan anayehusika na usalama na utulivu kuendeleza kipindi cha mpito cha Sudan kuelekea demokrasia na kuheshimu matakwa ya watu."Jeshi lawakamata mawaziri wanne Sudan
Chama cha wanataaluma cha Sudan ambacho ni mwamvuli wa vyama vya wafanyakazi ambavyo vilikuwa muhimu katika maandamano ya mwaka 2019 ya kumpinga Bashir, kimeshutumu kile walichokiita "mapinduzi ya kijeshi" na kuwataka waandamanaji kupinga vikali hatua hiyo.
Hayo yanatokea siku mbili baada ya kundi la Sudan linalotaka mamlaka kuhamishiwa kwa raia kuonya juu ya "mapinduzi" katika mkutano na waandishi wa habari ambao ulivamiwa na kundi la watu wasiojulikana. Sudan imekuwa katika kipindi cha mpito cha tahadhari kilichogubikwa na mgawanyiko wa kisiasa na kuwania madaraka tangu Bashir alipoondolewa mamlakani mwaka 2019.
Bashir ambaye aliitawala Sudan kwa mkono wa chuma kwa miongo mitatu yuko jela mjini Khartoum katika gereza lenye ulinzi mkali. Rais huyo wa zamani kwa muda mrefu alikuwa akitakiwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC kwa zaidi ya muongo mmoja kwa makosa yanayohusiana na mauaji ya kimbari na uhalifu wa kivita katika mkoa wa Darfur. Tangu mwaka 2019, Sudan imeongozwa na utawala wa kiraia na kijeshi uliokuwa na jukumu la kuirejesha nchi katika utawala kamili wa kiraia.