1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mamia wapoteza maisha kufuatia mafuriko Kongo

11 Januari 2024

Mamlaka za Kongo Kinshasa na Kongo-Brazzaville zimesema watu 300 wamepoteza maisha kufuatia mafuriko yaliyosababishwa na kupanda kwa kiwango cha maji ya Mto Kongo.

DR Kongo |
Kaya 300,000 zimeathirika nchini DRC kufuatia mafuriko ambayo mafuriko yaliyosababishwa na kupanda kwa kiwango cha maji katika Mto Kongo.Picha: Xinhua/IMAGO

Ubovu wa miundombinu na upangaji wa kiholela wa miji unatajwa kuwa sababu kuu inayopelekea baadhi ya mataifa ya kiafrika kukumbwa na mafuriko makubwa ya mara kwa mara kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Soma zaidi: Mahakama ya katiba ya Kongo yathibitisha ushindi wa Tshisekedi

Ferry Mowa, mtaalamu anayehusika na masuala ya mito na maji nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema ofisi yake ilitoa tahadhari ya kupanda kwa kiwango cha maji mwezi desemba mwaka uliopita na ikaonya kuwa ni lazima watu kuchukua tahadhari kwa kuwa ukanda mzima wa mto Congo unaweza kuathirika na mafuriko. 

Kiwango cha maji kwenye mto Kongo kilifikia mita 6.2 kutoka usawa wa bahari ikiwa ni pungufu ya alama kidogo ikilinganishwa na mita 6.26 iliyorikodiwa mnamo mwaka 1961.Picha: MARCO LONGARI/AFPGetty Images

Mtaalam huyo ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa siku ya Jumatano ya wiki hii, mto Kongo ulifikia mita 6.20 juu ya usawa wa bahari, kiwango ambacho kidogo kifikie rekodi ya mwaka 1961 ya mita 6.26 na hii ni kutokana na ongezeko la mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.
Wizara inayoshughulikia masuala ya kijamii nchini   Jamahuri ya kidemokrasia ya Congo imesema kuwa vitongoji kadhaa katika mji mkuu wa Kinshasa wenye idadi kubwa ya watu wengi nchini humo vimeathirika pakubwa pamoja na jamii zingine zilizopo pembezoni mwa mto huo.

Maelfu wapoteza makaazi 

Kongo imekuwa ikikabiliwa na mafuriko ya mara kwa mara na hii ni kutokana na miundombinu duni na upangaji wa kiholela wa miji.Picha: GLODY MURHABAZI/AFP

Taarifa hiyo ya wiki iliyopita iliongeza kuwa karibu watu 300 wamepoteza maisha na kaya 300,000 zimeharibiwa tangu wiki iliyopita.

Katika nchi jirani ya Kongo Brazaville,  mji mkuu wake Brazzaville ambao unapitiwa na mto Congo inatajwa kuwa watu 17 wamepoteza maisha na nyumba zaidi ya 60,000 kuathirika kutokana na mafuriko hayo.

Baadhi ya wakazi sasa wanatumia majembe kupiga kasia katika mitaa iliyofurika maji ambapo maji yamepanda hadi kiwango cha paa la baadhi nyumba. 

Katika manispaa ya Ngaliema magharibi mwa Kinshasa, Hellen ambaye mkazi mmoja wa eneo hilo amesema hawaja shuhudia hali kama hiyo.

''Tumeishi katika mtaa huu tangu tukiwa watoto, na ni mara ya kwanza tangu kuzaliwa kwetu kukumbwa na hali hii, hivyo ili kuzunguka inabidi kutumia mitumbwi, na tunaendelea kuishi katika hali hii kwa sababu sina mahali pengine pa kwenda.", alisema Hellen. 

Waathirika wahitaji misaada

Raphael Tshimanga Muamba, mkurugenzi wa utafiti wa Bonde la Kongo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ametoa wito wa kutolewa kwa msaada wa haraka ili kukabiliana na majanga ya asili na mabadiliko ya tabia ya nchi.

Kwa upande wake Waziri wa masuala ya kijamii na misaada ya kibinadamu nchini humo,Modeste Mutinga, ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa watafanya mkutano alhamisi hii kutathmini misaada zaidi ya kibinadamu.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW