1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mamia ya mahujjaji wafa Makka kwa joto kali

19 Juni 2024

Mamia ya mahujjaji wameripotiwa kufariki wakati wa ibaada ya mwaka huu nchini Saudi Arabia kutokana hasa na joto kali nchini humo, maafisa wamesema Jumatano huku watu wakitafuta maiti za wapenda wao.

Saudi Arabia | Vifo kutokana na joto kali katika Hijja
Hijja ya mwaka huu imefanyika katikati mwa hali ya joto kaliPicha: FADEL SENNA/AFP/Getty Images

Saudi Arabia haijazungumzia idadi ya vifo hivyo vilivyotokea katikati mwa joto kali wakati wa hijja, wala kutoa sababu zozote kwa waliofariki, lakini mamia ya watu walikuwa wamejipanga kwenye Jengo la Dharura katika kitongoji cha Al-Muaisem mjini Makka, wakijaribu kupata taarifa kuhusu wanafamilia wao waliopotea. Orodha moja inayosambaa mtandaoni iinaonyesha takriban watu 920 walikufa wakati wa Hijja, kulingana na ujumuishaji wa shirika la habari la AFP, wa hesabu zilizotolewa na mataifa mbalimbali.

Mhudumu mmoja wa afya aliyezungumza na shirika la habari la The Associated Press kwa sharti la kutotajwa jina ili kuzungumzia habari ambazo hazijatolewa hadharani na serikali, alisema kuwa majina yaliyoorodheshwa yalionekana kuwa ya kweli. Daktari huyo na afisa mwingine ambaye pia alizungumza kwa sharti la kutotajwa jina walisema wanaamini kuwa angalau miili 600 ilikuwa katika kituo hicho.

Mahujjaji wakijikinga na miavuli kutokana na jua kaliPicha: FADEL SENNA/AFP/Getty Images

Vifo ni jambo la kawaida katika Hijja, ambayo mara kwa mara inawavuta zaidi ya watu milioni mbili kwenda Saudi Arabia. Kumekuwa na mikanyagano na magonjwa ya milipuko katika historia yote ya ibaada ya Hijja ambayo ni nguzo ya tano ya Uislamu, iliyo wajibu kwa kila Muislamu mwenye uwezo kuitekeleza alau mara moja katika maisha yake.

Soma pia: Mahujjaji wakusanyika Arafat katika kilele cha Hijja

Kila mwaka, Hijja huvutia mamia ya maelfu ya mahujaji kutoka mataifa maskini, "wengi wao wakikuwa na huduma ndogo ya afya kabla ya Hijja," iliandikwa katika makala ya toleo la Aprili la Jarida la Maambukizi na Afya ya Umma.

Magonjwa ya kuambukiza yanaweza kuenea miongoni mwa umati uliokusanyika, ambao wengi wao waliweka akiba kwa muda mrefu sana kwa ajili safari hiyo na wanaweza kuwa wazee walio tayari na hali dhofu za kiafya kabla ya safari hiyo, iliongeza makala hiyo.

Joto lililopindukia laelezwa kuwa chanzo kikuu

Hata hivyo idadi ya vifo mwaka huu inaonyesha kuwa kuna kitu kilisababisha idadi hiyo kuongezeka. Tayari, nchi kadhaa zimesema baadhi ya mahujaji wao walikufa kwa sababu ya joto kali lililoyakumba maeneo matakatifu ya Makka, zikiwemo Jordan na Tunisia.

Siku ya Jumanne halijoto ilifikia nyuzi 47 za selisias mjini Makka na maeneo matakatifu ndani na karibu na jiji hilo, kulingana na Kituo cha Kitaifa cha Utabiri wa Hali ya Hewa cha Saudia. Watazamaji waliona baadhi ya watu wakizirai katika tukio la kiishara la kumrushia mawe shetani. Katika Msikiti Mkuu wa Makka, joto lilifikia nyuzi 51.8 C siku ya Jumatatu ingawa mahujaji walikuwa tayari wameondoka kuelekea Mina, walisema maafisa.

Mahema ya mahujjaji yakiwa yametanda aktika viwanja vya Mina, karibu na Mji Mtakatifu wa Makka, wakti wa ibaada ya Hijja ya mwaka 2024.Picha: Rafiq Maqbool/AP Photo/picture alliance

Wengine, wakiwemo Wamisri wengi, walipotezana na wapendwa wao katika joto na umati wa watu. Zaidi ya Waislamu milioni 1.83 walifanya ibada ya Hija mwaka 2024, wakiwemo mahujaji zaidi ya milioni 1.6 kutoka nchi 22, na takriban raia 222,000 wa Saudia na wakaazi, kwa mujibu wa mamlaka ya Hijja ya Saudi Arabia.

Siku ya Jumatano katika hospitali ya Makka, mwanamume mmoja raia wa Misri alianguka chini aliposikia jina la mama yake miongoni mwa waliofariki. Alilia kwa muda kabla ya kunyanyua simu yake ya mkononi na kumpigia wakala wa usafiri, huku akipiga kelele: "Alimwacha afe!" huku umati ukijaribu kumtuliza mtu huyo.

Mabilioni ya dola kudhibiti usalama katika Hijja

Hali ya ssalama ilionekana kuimarishwa pakubwa katika jengo la hospitali hiyo, waakti afisa akisoma majina ya waliofariki na utaif wao, ambao walihusisha mahujjaji kutoka Algeria, Misri na India. Waliosema ni ndugu wa waliofariki waliruhusiwa kuingia ndani ili kutambua marehemu.

Soma pia: Mahujaji milioni mbili waanza safari ya Arafa

Watawala wa ufalme huo, familia ya Al Saud wanadumisha ushawishi mkubwa katika ulimwengu wa Kiislamu kupitia utajiri wake wa mafuta na usimamizi wa maeneo matakatifu zaidi ya Uislamu. Kama wafalme wa Saudia waliomtangulia, Mfalme Salman ametwaa cheo cha Mlinzi wa Misikiti Miwili Mitakatifu - Msikiti wa Makka iliko Kaaba ambako Waislamu huelekea mara tano kwa siku wakati wakiswali, na Msikiti wa Mtume katika mji wa karibu wa Madina.

Saudi Arabia inatumia mabilioni ya dola kuweka miundombinu ya kudhibiti umati na kuimarisha usalama kwa wanaohudhuria Hijja ya kila mwaka, lakini idadi kubwa ya washiriki inafanya uhakisho wa usalama wao kuwa mgumu.

Mahujaji waelekea Mlima Arafat Makka

01:07

This browser does not support the video element.

Mabadiliko ya tabianchi yanaweza kufanya hatari kuwa kubwa zaidi. Utafiti wa 2019 uliofanywa na wataalamu katika Taasisi ya Teknolojia ya Massachusetts uligundua kuwa hata kama ulimwengu utafanikiwa kupunguza athari mbaya zaidi za mabadiliko ya tabianchi, Hijja itafanyika katika hali ya joto inayovuka "kizingiti cha hatari zaidi" kuuanzia mwaka 2047 hadi 2052, na kutoka 2079 hadi 2086.

Uislamu unafuata kalenda ya mwezi, kwa hivyo Hijja hufanyika karibu siku 11 mapema kila mwaka. Mnamo 2030, Hajj itatokea Aprili, na kwa miaka kadhaa ijayo itaanguka wakati wa baridi, wakati ambapo hali ya joto inakuwa ya wastani.

Soma pia:Ibada ya Hijja yaanza chini ya kiwingu cha COVID-19

Mkanyagano wa mwaka 2015 huko Mina wakati wa Hijja uliua zaidi ya mahujaji 2,400, tukio baya zaidi kuwahi kutokea kwenye ibada ya Hijja. Saudi Arabia haijawahi kutangaza winchi kamili ya vifo vilivyotokana na mkanyagano huo. Tukio tofauti la kuporomoka kwa kreni katika Msikiti Mkuu wa Makka, lililotangulia maafa ya Mina, liliuwa watu 111.

Tukio la pili baya zaidi wakati wa Hijja lilikuwa mkanyagano wa mwaka 1990 ambamo watu 1,426 waliuawa.

Chanzo: Mashirika

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW