1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mamia ya raia wa kigeni waingia Misri kutokea Gaza

2 Novemba 2023

Kundi la kwanza la watu waliojeruhiwa wameondoka Gaza na kuingia Misri kupitia kivuko cha Rafah huku pia raia wa kigeni nao wakiendelea kuvuka mpaka

Gazastreifen Rafah Grenzübergang zu Ägypten
Picha: Arafat Barbakh/REUTERS

Kufikia jana jioni, zaidi ya raia 300 wa kigeni na watu wenye uraia pacha waliingia Misri kupitia kivuko cha Rafah. Ndio kundi la kwanza kuondoka Gaza chini ya mpango kati ya Misri, Israel na Hamas uliosimamiwa na Qatar kwa ushirikiano na Marekani. Hayo ni kwa mujibu wa duru za usalama za Misri na afisa mmoja wa Kipalestina.

Soma pia: Misri yawapokea majeruhi kutoka Ukanda wa Gaza

Rais wa Marekani Joe Biden alisema katika ujumbe alioandika kwenye mtandao wa X ukifahamika awali kama Twitter, kuwa raia wa Marekani watakuwa miongoni mwa watu wanaondoka Gaza kuanzia jana akiongeza kuwa wanatarajia kuona idadi hiyo ikiongezeka katika siku chache zijazo.

Israel imeipiga kambi ya wakimbizi ya JabaliyaPicha: Mohammed Al-Masri/REUTERS

Miongoni mwa waliokuwa katika kundi hilo ni raia wa Italia, raia watano wa Ufaransa na raia kadhaa wa Ujerumani. Maafisa kutoka nchi hizo tatu waliandika kwenye mtandao wa X. Kiasi raia 500 wenye paspoti za kigeni walitarajiwa kuvuka mpaka na kuingia Misri jana, kwa mujibu wa maafisa wa Misri. Mapema jana, kundi la kwanza la Wapalestina waliojeruhiwa walisafirishwa hadi Misri na kupelekwa katika hospitali iliyo karibu kwa matibabu.

Jeshi la Israel lamuuwa kamanda mwingine wa Hamas

Katika Ukanda wa Gaza kwenyewe, vikosi vya Israel vimemuuwa leo kamanda mwingine wa Hamas katika shambulizi lao la pili kwenye kambi kubwa kabisa ya wakimbiizi ya Jabaliakatika kipindi cha siku mbili. Huku wakiendelea na operesheni yao dhidi ya wanamgambo wa Hamas, Israel iliendelea kudondosha mabomu katika ukanda huo kutokea ardhini, majini na angani. Hakujawa na taarifa yoyote ya mara moja kuhusu idadi ya vifo au majeruhi kutokana na mlipuko wa pili, ambao umejiri siku moja baada ya maafisa wa afya wa Palestina kusema shambulizi la angani la Israel liliwauwa watu 50 na kuwajeruhi 150.

Malori ya msaada yanaendelea kuingia kusini mwa GazaPicha: Ahmad Hasaballah/Getty Images

Soma pia: Guterres: Kuna hatari ya kutanuka mzozo wa Israel na Hamas

Jeshi la Israel lilitoa taarifa ikisema ndege zake za kivita zilikipiga kutuo cha kamandi cha Hamas katika kambi ya wakimbizi ya Jabalia kwa kuzingatia taarifa za kijasusi, na kumuuwa kiongozi wa kitengo cha vuguvugu hilo cha kupambana na mashambulizi ya vifaru, Muhammad A'sar. Israel ilisema shambulizi la Jumanne kwenye kambi hiyo hiyo lilimuuwa Ibharim Biari, ambaye lilisema alikuwa mhusika mkuu wa shambulizi la kigaidi lililofanywa na Hamas Oktoba 7 ndani ya Israel.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binaadamu imesema mashambulizi ya Israel kwenye kambi hiyo ya wakimbizi Gaza yanaweza kufikia kiwango cha uhalifu wa kivita. Ofisi hiyo imeandika kwenye mtandao wa X kuwa kutokana na idadi kubwa ya vifo vya raia na kiwango cha uharibifu kufuatia mashambulizi ya Israel kwenye kambi ya wakimbizi ya Jabalia, ina wasiwasi mkubwa kuwa mashambulizi hayo yasiyo na uwiano yanaweza kuwa ni uhalifu wa kivita.

Israel inaendelea na operesheni ya ardhini wa GazaPicha: Israel Defense Forces/Handout via REUTERS

Jeshi la Israel lasema lipo kwenye milango ya Mji wa Gaza

Wakati huo huo askari wa Israel wanaendelea na operesheni yao kubwa ya ardhini katika Ukanda wa Gaza na wanaukaribia Mji wa Gaza. Kamanda wa kikosi hicho Itzik Cohen amewaambia waandishi Habari kuwa "wamesimama katika milango ya Mji wa Gaza.”

Amesema wanajeshi wako Gaza na wameuharibu uwezo wa Hamas na kushambulia vituo vya kimkakati.

Jeshi la Israel limesema jumla ya askari wake 16 wameuawa katika mapigano tangu Jumanne katika makabiliano ndani na karibu na Ukanda wa Gaza.

afp, ap, reuters, dpa