1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mamia ya wahamiaji wengine wafa maji

30 Mei 2016

Zaidi ya wahamiaji 700 wanahofiwa kufa maji katika Bahari ya Mediterenia kutokana na kuzama kwa mashua zao wiki iliopita licha ya kwamba meli za uokozi zimewaokoa maelfu ya wengine katika operesheni ngumu kabisa.

Picha: picture alliance/dpa/SOS MEDITERRANEE

"Nataka kuiambia dunia kwamba njia hii hatari sana kwetu kwa sababu kaka yangu, dada yangu watakuja kupoteza maisha yao katika mkondo huu wa bahari.Tafadhali tusaidieni tuwe na uhuru katika nchi yetu . Sitaki kubakia hapa au mahala pengine popote pale.Nataka nchi yangu iwe na uhuru."

Hiyo ni kauli ya Habtom Tekle raia wa Eritrea mwenye umri wa miaka 27 akiwa ni miongoni mwa wahamiaji walionusurika katika janga la kuzama kwa mashua za wahamiaji wiki iliopita katika bahari ya Mediterenia na kusababisha maafa ya mamia ya wahamiaji.

Kuzama kwa mashua zao hizo kumesababisha idadi kubwa ya vifo kutokea katika Bahari ya Mediterenia tokea maafa ya mwezi wa Aprili mwaka 2015 ambapo mashua moja ilizama ikiwa na wahamiaji 800.

Mashua zinazama bila kujulikana

Mashirika ya misaada ya kibinaadamu yanasema mashua nyingi za wahamiaji zinazama bila ya kugundulikana na watu waliokufa kutopatikana kabisa isipokuwa majaaliwa yao kuja kujulikana baada ya familia zao kuripoti kwamba hawakuwasili Ulaya walikokuwa wakiwatarajia.

Helikopta katika harakati za uokozi baharini kati ya Libya na Italia.Picha: picture-alliance/dpa/Italian Navy/Marina Militare

Bahari iliyo shwari pamoja na utulivu wa hali ya hewa hivi karibuni kumesababisha kuongezeka kwa idadi ya wahamiaji wanaojaribu kukimbilia Ulaya.

Idadi kubwa ya wahamiaji wasiojulikana walipo na wanaodhaniwa kuwa wamekufa walikuwa kwenye mashua ya uvuvi iliokuwa ikiburuzwa na mashua nyengine ya kusafirisha watu kwa magendo kutoka bandari ya Sabratha nchini Libya iliyozama Alhamisi.

Makadirio ya maafa

Makadirio ya polisi na mashirika mengine ya misaada ya kibinaadamu kwa kuzingatia maelezo ya wahamiaji walionusurika, ni kuwa watu kati ya 400 hadi 500 hawajulikani walipo kutoka katika mashua hiyo iliyozama.

Wahamiaii kutoka Libya walioweza kuokolewa Italia.Picha: Getty Images/AFP/G. Isolino

Kwa mujibu wa polisi ya Italia, watu 300 waliokuwa katika eneo la chini katika mashua ya pili walizama na mashua yao hiyo, wakati wengine kama 200 waliokuwa sehemu ya juu ya mashua hiyo walichupa baharini, lakini ni 90 tu walioweza kuokolewa pamoja na wengine 500 waliokuwemo katika mashua ya kwanza.

Kwa mujibu wa shirika la kutetea watoto la Save the Children wengi wa wahamiaji walikuwa ni raia wa Eritrea, wakiwemo wanawake na watoto.

Uturuki yatishia kutelekeza makubaliano

Hayo yanajiri wakati serikali ya Uturuki ikitishia kuyatelekeza makubaliano na Umoja wa Ulaya ya kudhibiti wimbi la wakimbizi barani Ulaya, iwapo raia wake hawatoruhusiwa kusafiri barani Ulaya bila ya visa.

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki.Picha: Getty Images/AFP/A. Altan

Wakati pande hizo mbili zikiwa katika mvutano mkubwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu, amesema haiwezekani kwa serikali ya Uturuki kubadili sheria zake za kupambana na ugaidi ambazo Umoja wa Ulaya unataka zirekebishwe kama moja ya masharti ya kuondosha viza kwa Waturuki wanaoingia Ulaya.

Akitilia mkazo kauli ya Rais Recep Tayyip Erdogan wiki iliyopita, waziri huyo amesema ikibidi Uturuki itachukuwa hatua za kiutawala kukwamisha makubaliano hayo.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP/AP

Mhariri: Mohammed Khelef

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW