Mamia ya wakimbizi wahofiwa kuzama Mediterenia
19 Aprili 2015Antonio Irato afisa mwandamizi wa polisi wa mapakani wa Italia amekiambia kituo cha televisheni cha RaiNews24 kwamba watu 28 wameokolewa katika ajali hiyo ambayo imetokea nje kidogo ya bahari ya Libya na kusini mwa kisiwa cha Lampedusa nchini Italia.Amesema maiti 49 zimepatikana
Iwapo idadi ya maafa itathibitika jumla ya watu walipoteza maisha kuingia Ulaya kwa njia hiyo ya bahari ya Medirerania tokea kuanza kwa mwaka huu itapindukia 1,500.
Maafa hayo yanachochea wito wa kutaka Ulaya ichukuwe hatua madhubuti zaidi kukabiliana na mzozo wa uhamiaji unaozidi kusababisha maafa katika bahari ya Mediterania. Mashirika ya misaada ya kimataifa na serikali ya Italia imeshutumu kile kinachojulikana kama "Triton" operesheni ya kulinda mipaka ya Ulaya ambayo hivi karibuni imechukuwa nafasi ya operesheni ya Italia ambayo ilikuwa kabambe zaidi ya kutafuta na kuokowa wahamiaji.
Maafa yasifumbiwe macho
Waziri Mkuu wa Malta Joseph Muscat amesema maafa yanatokea Mediterania na iwapo Umoja wa Ulaya na dunia zitaendelea kufumba macho yao itathminiwa vibaya kama ilivyotathminiwa hapo zamani wakati ilipofumbia macho mauaji ya kimbari ambapo walipakata mikono bila ya kuchukuwa hatua yoyote ile.
Serikali ya Italia imesema meli za ulinzi wa mwambao na manowari halikadhalika meli za kibiashara katia eneo hilo na mashua ya doria ya Malta zinahusika katika operesheni ya kuwatafuta na kuwaokowa wahamiaji hao ambayo inaratibiwa na kikosi cha majini cha Italia mjini Rome.Ameongeza kusema kwamba wanajaribu kuwapata wakiwa hai miongoni mwa miili inayoelea baharini.
Inaaminika kwamba mashua hiyo ilipinduka na kuzama wakati wahamiaji waliokuwemo ndani walipoelemea upande mmoja wa mashua hiyo iliofurika watu wakati ilipokuwa ikisogelewa na meli ya kibishara ya Ureno.
Chanzo cha ajali
Maelezo hayo yametolewa na mmojawapo wa watu walionusurika anayezungumza Kingereza ambaye amesema takriban watu 700 na pengine hata zaidi waliokuwemo ndani ya chombo hicho.
Carlota Sami msemaji wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR amemnukuu manusura huyo akisema mashua hiyo imezama kwa sababu watu waliegemea upande mmoja wakati meli nyengine ambayo walitegemea ingewaokowa ilipokuwa ikiwasogelea.
Waziri Mkuu wa Italia Matteo Renzi amesema wanashuhudia mauaji ya umma mzima wa watu katika bahari ya Mediterania.Akizungumza katika hafla ya kisiasa huko Mantua ameuliza "Vipi wanaweza kuendelea kutojali wakati wakishuhudia umma mzima unapoteza maisha katika enzi ambapo nyezo za kisasa za mwasiliano zinawawezesha kutambuwa kila kitu?"
Renzi alizungumza kwa simu juu ya kadhia hiyo na Rais Francois Hollande wa Ufaransa.
Udhibiti uanzie Libya
Kiongozi wa chama cha "Ligi ya kaskazini" Nothern League cha Italia chenye kupinga uhamiaji Matteo Salvini ambaye amelifanya suala la uhamiaji kuwa mojawapo ya mada kuu za agenda yake ya kisiasa ametowa wito wa kuwekwa mara moja kwa vizuizi vya majini kuufunga mwambao wa Libya.
Libya nchi ambayo imekuwa haina utawala wa sheria kufuatia kupinduliwa kwa kiongozi wa zamani wa nchi hiyo Muammer Gaddafi hapo mwaka 2011 imeayaacha magenge ya uhalifu yanayosafirisha wahamiaji kwa magendo kujifanyia wanavyotaka na kupeleka mkururo wa mashua zenye kubeba wahamiaji wanaotapia maisha kutoka Afrika na Mashariki ya Kati.
Mwaka huu, hadi sasa zaidi ya zaidi ya watu 900 wamefariki wakati wakijaribu kuvuka bahari ya Mediterania kuingia Ulaya.Wiki iliopita watu 400 inaaminika kuwa wamekufa wakati mashua yao ilipozama.
Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters//AP
Mhariri :Hamidou Oummilkheir