1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Cameroon Chad: Mamia ya watu waathirika na mafuriko

25 Oktoba 2022

Maafisa wa Cameroon na Chad wanasema zaidi ya raia wao laki moja walioyahama makazi yao kutokana na mafuriko mabaya ya mwezi huu wanatafuta msaada bila mafanikio katika pande zote za mpaka wao wa pamoja.

BG Überschwemmungen | Tchad
Picha: Mahamat Ramadane/REUTERS

Mwandishi wa DW huko Younde Moki Edwin Kindzeka anaripoti kuwa mafuriko yamechochea wimbi jipya la mlipuko wa kipindupindu hadi kwenye kambi za wakimbizi.

Rais wa Cameroon, Paul BiyaPicha: AP

Rais wa Cameroon Paul Biya wiki iliyopita alimtuma waziri wa utawala wa maeneo Paul Atanga Nji ili kutathmini mahitaji ya kibinadamu ambayo waathiriwa walisema hayatoshi. Rais wa Chad Mahamat Idriss Deby kwa upande wake alitangaza hali ya hatari kutokana na mafuriko.

Mvua imekuwa ikinyesha kwa wiki moja mfululizo huko Kousseri, mji ulio kwenye mpaka wa kaskazini mwa Cameroon na Chad. Mvua kubwa husababisha mto wa Logone, unaozigawa nchi hizo mbili, kufurika.

Zaidi ya watu laki moja wamekimbia makazi yao. Raia 70,000 hawana makazi. Njaa imetanda huku mashamba na wanyama vikisombwa na mafuriko.

Mada zinazohusiana: 

Athari kubwa ya mafuriko Chad

01:21

This browser does not support the video element.

Madou Simon Pierre, kasisi wa kanisa katoliki katika mji mkuu wa Chad N'Djamena anasema mamia ya watu waliokimbia makazi yao, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wanatafuta hifadhi makanisani. Anaeleza jinsi hali ilivyokuwa mbaya hivi sasa.

"Serikali ya Chad ilishindwa kujiandaa na mafuriko kwa sababu ilijikita katika kutatua mzozo wa kisiasa. Nilipotoa tahadhari mwezi uliopita kuwa maji yanaongezeka, viongozi wa Chad walisema Baba mchungaji, tunajishughulisha na mazungumzo ya kitaifa. Ndiyo sababu tunajikuta wenyewe katika hali hii"

Mamia ya watu wanapokea matibabu baada ya wimbi jipya la kipindupindu kukumba eneo hilo. Watu wasiopungua 22 wamefariki na wengi zaidi wanahofiwa kukutwa na mauti katika maeneo ambayo ni vigumu kuyafikia.

Soma zaidi: Kiongozi wa Chad atangaza hali ya hatari kufuatia mafuriko

Siku ya Jumapili, Shirika la Kimataifa la kuwahudumia Wakimbizi UNHCR lilitaja kuhuzunishwa mno na vifo vya wakimbizi watatu kati ya 81 waliothibitishwa kuambukizwa kipindupindu huko Minawao, kambi ya wakimbizi ya Nigeria. Kambi hiyo ina Wanigeria 76,000 wanaokimbia ugaidi wa Boko Haram.

Helen Ngoh, msemaji wa UNHCR nchini Cameroon anasema shirika hilo la Umoja wa Mataifa linahitaji msaada ili kuzuia na kudhibiti milipuko ya siku zijazo katika kambi ya wakimbizi.

" Katika kambi ya Minawao pekee UNHCR inahitaji angalau Dola za Marekani 450,000 ili kuweza kuongeza usambazaji wa maji na pia kuweza kuziba pengo lililopo la vyoo 900 na kuweza pia kuboresha udhibiti wa taka kambini. Mahitaji haya yote ni ya muhimu sana kwa wakati huu."

Soma zaidi: Nusu ya nchi duniani hazina mifumo ya tahadhari ya majanga

Mtoto aliyekutwa na ugonjwa wa kipindupindu akifanyiwa vipimo na Daktari.Picha: Tsvangirayi Mukwazhi/AP/picture alliance

Umoja wa Mataifa unaripoti kuwa zaidi ya maambukizi 1,000 ya kipindupindu yaliripotiwa katika nchi jirani ya Nigeria yenye mpaka na Cameroon na Chad.

Linda Esso, mkurugenzi wa magonjwa ya milipuko katika Wizara ya Afya ya Umma ya Cameroon anasema hospitali katika maeneo ya mpakani zimezidiwa.

"Hatuwezi kusema kwamba wimbi la sasa la maambukizi ya kipindupindu linatoka Nigeria kwa sababu nchi jirani iliripoti mlipuko baada ya mafuriko makubwa ya mwezi huu. Kuna uwezekano kwamba baadhi ya raia walioambukizwa au walioathiriwa na mlipuko huo wanahamia hospitali zinazoweza kufikiwa pande zote mbili za mpakani kutafuta msaada. Kipindupindu kwa sasa kinaenea kupitia bonde la ziwa Chad kwa urahisi."

Soma zaidi:Vita vya Cameroon vilivyosahaulika vyawaacha wakimbizi njiapanda 

Esso amesema mlipuko wa kipindupindu unaenea kwa kasi katika maeneo ya bonde la Ziwa Chad ambalo linazijumuisha Cameroon, Chad, Nigeria, Niger na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Serikali ya Cameroon inasema imeshiriki katika majadiliano na Nigeria pamoja na Chad ili kukabiliana na kadhia hiyo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW