Mamia ya watu wanahitaji kuhamishwa kutoka Madaya
12 Januari 2016Mabalozi wa Umoja wa Mataifa wamesema mamia ya raia wanahitaji kusafirishwa kwa dharura kutoka mji huo ili kupokea huduma za matibabu. Hapo jana, msafara wa malori 44 ya kusafirisha vyakula na mahitaji mengine ya kimsingi ya Umoja wa Mataifa uliruhusiwa kuingia katika mji huo.
Malori mengine 21 yaliwasili katika miji mingine miwili Fuaa na Kafraya inayodhibitiwa na waasi na ambako pia raia wanakumbwa na njaa kali. Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lilifanya mkutano wa faragha kujadili hali hiyo ya raia kukwama katika miji kadhaa nchini Syria, ambako inaripotiwa raia wamelazimika kula nyasi na paka ili kuendelea kuishi.
Syria yawashutumu waasi
Balozi wa Syria katika Umoja wa Mataifa Bashar Jafaar amekanusha ripoti hizo na kuwashutumu waasi aliowataja magaidi kwa kuiba misaada ya chakula inayofikishwa katika mji wa Madaya.
Mkuu wa shirika la kutoa misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa Stephen O'Brien ameliambia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuwa Wasyria mia nne wako katika hali mbaya sana na iwapo hawataondoelewa kutoka Madaya usiku wa kuamkia leo, huenda hali yao ikazorota hata zaidi.
Uingereza na Ufaransa zinataka kukomesha kuzingirwa kwa miji hiyo. Balozi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa Mathew Rycroft amesema kuwanyima raia chakula ili wakabiliwe na njaa kubwa ni silaha katili inayotumika na utawala wa Rais Bashar al Assad na washirika wake.
Umoja wa Mataifa umesema unapambana kuwasilisha misaada kwa takriban Wasyria milioni 4.5 wanaoishi katika maeneo ambayo ni vigumu kuyafikia.
Huku hayo yakijiri, Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema Syria inahitaji kuanza mchakato wa kutafuta katiba mpya kama hatua ya kwanza ya kutafuta suluhisho la kisiasa la kuvimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Putin ataka katiba mpya Syria
Kiongozi huyo wa Urusi pia ameliambia gazeti la Ujerumani la Bild kuwa mzozo kati ya Saudi Arabia na Iran utahujumu mchakato wa kutafuta amani Syria. Vile vile amesema ni mapema mno kuzungumzia iwapo atampa hifadhi ya kisiasa Rais wa Syria Bashar Al Assad.
Putin ambaye ni mshirika wa karibu wa Assad amesema baada ya kupatikana kwa katiba mpya na uchaguzi ujao uendeshwe kwa njia ya kidemokrasia, Assad hahitaji kwenda kokote hata kama atashindwa katika uchaguzi huo.
Urusi, Marekani na nchi za Mashariki ya kati yanahimiza kuwepo mazungumzo kati ya serikali ya Syria na upinzani lakini kuendelea kuwepo madarakani kwa Assad kunaonekana kuwa suala tete.
Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga