1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mamia ya watu wauawa katika mashambulio nchini Msumbiji

29 Machi 2021

Mamia ya watu wameuawa katika mashambulio yaliyofanywa na kundi la wanamgambo wanaojiita dola la kiislamu IS katika mji wa Palma Kaskazini mwa Msumbiji na kusababisha kuhamishwa kwa maelfu ya watu hadi Pemba

BG I Alltag und Militarismus in Cabo Delgado
Picha: Roberto Paquete/DW

Siku ya Jumapili, msemaji wa jeshi Omar Saranga alisema kuwa mamia ya watu waliuawa ikiwa ni pamoja na watu saba waliouawa wakati msafara wao wa magari ulipovamiwa walipokuwa wakijaribu kukimbia kutoka eneo hilo lenye machafuko. Raia kadhaa wa kigeni pia wamenaswa katika vurugu hizo na serikali haijasema ni wangapi waliouawa. Kufikia sasa, ni raia mmoja tu wa Afrika Kusinialiyetambulika kuuawa baada ya familia yake kulithibitishia shirika la habari la  AFP.

Saranga amesema, mamia ya watu wengine wanaojumuisha raia wa nchi hiyo na wa kigeni pia waliokolewa kutoka mji huo ulio karibu na miradi ya gesi ya thamani ya dola bilioni 60. Saranga amefahamisha kuwa katika siku tatu zilizopita, vikosi vya ulinzi vya serikali vimetoa kipaombele kwa uokoaji wa mamia ya raia wa nchi hiyo na wa kigeni bila ya kutoa idadi kamili. Baadhi ya watu walipelekwa kwa muda katika kiwanda cha gesi kilicho chini ya ulinzi mkali kilichoko katika rasi ya Afungi  katika mpaka wa Tanzania ulioko Kusini mwa bahari hindi kabla ya kuhamishwa na kupelekwa Pemba, eneo la umbali wa kilomita 250 Kusini mwa Palma.

Wakazi wa Palma mkoani Cabo Delgado nchini MsumbijiPicha: Roberto Paquete/DW

Kwa mujibu wa polisi wanaoshika doria katika mji huo wa bandari, boti iliyokuwa imewabeba watu hao iliwasili Pemba hapo jana ikiwa na takriban watu 1400. Maafisa wa uwanja wa ndege wa Pemba wamesema kuwa safari za ndege za misaada zilikuwa zimesimamishwa ili kutoa nafasi kwa operesheni za kijeshi.

Martin Ewi , mtafiti mkuu wa kituo cha utafiti wa elimu ya ulinzi yenye makao yake Pretoria, amesema kuwa zaidi ya wati 100 bado hawajulikana walipo tangu mashambulio hayo kuanza na kuongeza kuwa hali katika eneo hilo ni ya kutatanisha.

Siku ya Jumatano, idadi isiyojulikana ya wanamgambo hao walianza kushambulia mji wa Palma katika mkoa wa Cabo Delgado ulio na idadi ya takriban wakazi elfu 75 na ambalo pia ni eneo la mradi mkubwa wa gesi unaofanywa na kampuni ya Total ya Ufaransa na kampuni nyingine za kawi.

Shirika la kutetea haki la Human Rights Watch limesema kuwa wanamgambo hao waliwafyatulia watu risasi kiholela katika nyumba zao na barabarani.