Mamilioni wakabiliwa na njaa Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika
23 Februari 2006Mamia ya watu na maelfu ya mifugo tayari wamekufa kutokana na njaa katika mojawapo ya vipindi vibaya kabisa vya ukame kuwahi kushuhudiwa kwenye eneo hilo kwa miaka mingi baada ya mvua kushindwa kunyesha hapo mwezi wa Novemba mwaka jana.
Kenya,Somalia na Ethiopia ndio nchi zilizoathiriwa zaidi na ukame huo.
Shirika la misaada la Uingereza Oxfam limesema katika taarifa kwamba ahadi yakinifu zilizotolewa na nchi tajiri kugharamia mfuko wa michango ya fedha kukabiliana na tatizo kubwa la uhaba wa chakula Afrika Mashariki zimekuwa hazitekelezwi kwa haraka inavyostahiki.
Oxfam limesema itikio la wito huo wa msaada limepokea dola milioni 168 kwa ajili ya msaada wa dharura kutoka dola milioni 574 zilizoombwa huo ukiwa ni upungufu wa asilimia 68.
Nchini Kenya ambapo Umoja wa Mataifa unasema watu milioni tatu na nusu maisha yao yako hatarini ni dola milioni 18. 7 au asilimia 8.3 tu zimeahidiwa kutolewa kati ya dola milioni 225 zinazohitajika.
Somalia kumeahidiwa kutolewa msaada wa dola milioni 30 au kama asilimia 17 ya dola milioni 174 zilizooombwa.
Kwa mujibu wa Oxfam ni Ethiopia tu ambayo inakaribia kufikia malengo ya msaada ilioumba wa dola milioni 175 ambapo msaada wa dola milioni 137 umeahidiwa kutolewa na mwengine zaidi ukitarajiwa kutolewa.
Viwango vya utapia mlo kaskazini mwa Kenya ni zaidi ya maradufu ya asilimia 15 ambayo hali ya hatari hutangazwa.
Huko Turkana kaskazini magharibi ya Kenya baadhi ya familia zinaendelea kuishi kwa kutegemea matunda mwitu, wanyama aina ya kuchakuro au kindi na wadudu kutokana na ukosefu wa vyakula vengine.
Uhaba wa chakula umeshadidia mapigano makali kati ya makabila ya ufugaji ambayo hutanga tanga katika eneo hilo na Oxfam limesema kwamba nchini Somalia watoto wenye kiu hunywa mkojo wao wenyewe.
Nchini Burundi ambapo njaa imeuwa zaidi ya watu 250 Rais Piere Nkurunziza wiki hii ameamuru wafanyakazi wote wa Burundi kutowa baadhi ya mapato yao kwa kuchangia mfuko wa kusaidia kukabiliana na janga la njaa nchini humo.
Watu 250 wamekufa nchini Burundi kutokana na njaa tokea mwezi wa Desemba na watu 35 wamekufa wiki iliopita pekee na wengine zaidi ya 6,000 wamekimbilia nchi jirani ya Tanzania kukimbia ukame huo.
Mwakilishi mwandamizi wa Umoja wa Mataifa ametowa wito wa dharura kusaidia mamilioni ya watu wanaokabiliwa na janga la njaa Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika na kuonya kwamba watu tayari wanakufa njaa kutokana na hali mbaya kabisa ya ukame kwa baadhi ya sehemu za Afrika.
Kjell Magne Bondevik amesema hilo ni jambo zito sana na ni tatizo kubwa sana kwamba iwapo jumuiya ya kimataifa haitozinduka yatakuja kuwa maafa hasa.
Bondevik ambaye ni mwakilishi mpya wa masuala ya kibinadaamu wa Umoja wa Mataifa kwa Pembe ya Afrika na waziri mkuu wa zamani wa Norway alitembelea kusini mwa Kenya kujionea mwenyewe taathira ya ukame ambayo imelikumba eneo la mashariki,kati na Pembe ya Afrika.
Inaelezwa kwamba uharibifu wa misitu,janga la UKIMWI umaskini uliotopea,ukosefu wa uwekezaji vijijini na barabara mbovu ni mambo yanayoifanya Afrika iwe rahisi kuathirika na majanga kama hayo ya ukame na njaa.