1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiSomalia

Mamilioni wakabiliwa na uhaba wa chakula Somalia

12 Agosti 2026

Somalia inaandamwa na hali ngumu ya njaa na ukame katika mazingira ya changamoto zinazosababishwa na vita vya muda mrefu vilivyoathiri uchumi wa nchi hiyo huku maelfu wakielekea katika kambi za muda mjini Baidoa.

Afrika I Baa la njaa Somalia
Wanawake raia wa Somalia walioathirika na ukame wakiwa katika kambi ya muda ya Alla FutoPicha: Feisal Omar/REUTERS

Takriban watu milioni mbili wanakabiliana na uhaba mkubwa wa chakula mwaka huu ikilinganishwa na hali ilivyokuwa katika mwaka uliopita. Maelfu ya wasomali wanaokimbia njaa wamekusanyika kwenye kambi za muda katika mji wa Baidoa ulio kaskazini, magharibi ya mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Mji huo wa Baidoa kwa sasa umekuwa kituo muhimu kwa wanaokimbia madhila ya njaa,vurugu na uhaba wa chakula.

Safari ya wiki mbili, ya Luul Mohamed na wanawe watano waliowasili kwenye mji huo ni mfano wa jinsi Somalia inavyotatizwa na janga la kibinadamu ambalo athari zake zinaongezwa na ukame, vita na changamoto za kiuchumi.

"Tuna njaa na hali ni ngumu. Tumekuwa tukitembea kwa siku kadhaa, tukipata hifadhi kutoka kijiji kimoja hadi chengine mpaka tukawasili Baidoa jana jioni. Pindi tulipofika,mume wangu alienda kusaka kibarua kwenye mashamba ya wakaazi ili angalau tupate chakula cha watoto. Hayo ndiyo yanayotuzonga.Hatuna chakula na tunamtumainia Mola tu kwani ndiye anayetusitiri," amesema Luul Mohamed.

Familia nyingi zimelazimika kuvikimbia vijiji vyao na kuhamia kwenye kambi za muda wakati ambapo makali ya njaa yanaongezeka na misaada ya kibinadamu inanywea.

Mashirika yanaonya hatua za haraka zinahitajika kuzuia hali kuzorota zaidi

Takwimu zinaashiria kuwa kiasi ya watu milioni mbili wanakabiliana na uhaba mkubwa wa chakula, idadi ambayo ni maradufu ikilinganishwa na mwaka uliopita, linaelezea shirika la misaada la Plan International ambalo limewasaidia zaidi ya watu laki mbili huko Somalia mwaka huu pekee.

Ili kudhibiti hali, shirika hilo pamoja na shirika la serikali ya Somalia la kupambana na majanga yanaitolea wito jamii ya kimataifa kuiongezea msaada kwani madhila huenda yakaongezeka ukizingatia hali ya hewa.

Kwa upande wake, shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO, linatabiri kuwa uwezekano wa madhara ya El Nino kushuhudiwa katikati ya mwaka huu ni mkubwa kwa asilimi 90 na kitisho cha mafuriko kutokea katika msimu ujao wa mvua wa kati ya mwezi wa Oktoba hadi Disemba.

Somalia iko katika hatari ya kutatizwa na hali mbaya ya anga kwani imepitia vipindi virefu vya ukame unaofuatiwa na mafuriko. Madhila hayo yamevuruga biashara, kuwaacha baadhi bila makazi, kusababisha magonjwa kuzuka na kuuongeza uwezekano wa chakula kuadimika.

Huenda msaada wa chakula Somalia ukaisha katika wiki chache

01:25

This browser does not support the video element.

Mjini Baidoa,, hali si hali na maelfu wanaokimbia madhara ya ukame wa muda mrefu wamekusanyika kwenye kambi za muda pembezoni ya jiji. Kwa mujibu wa Plan International, Baidoa inawapa hifadhi watu wapatao milioni 1.6, nusu yao wakiwa wameyakimbia makaazi yao.

Reena Ghelani ni afisa mkuu mtendaji wa shirika la msaada la Plan International na alikuwa Baidoa hivi karibuni na hii ndiyo hali aliyokutana nayo.

"Niliwasiliana na baadhi…..watu ambao walikimbia baada ya kusubiri mwaka hadi mwaka wa madhila ya ukame na wanahangaika.Kwa sasa wanasema hawana chochote.Hakuna maji. Hawana chakula na bidhaa za matumizi.Mifugo yao pia imefariki.Hawana chochote kwa kweli..kwahiyo wamelazimika kuhama hatimaye."

Familia moja kati ya tano zinatatizwa na uhaba wa maji na wanalazimika kununua kutoka kwa malori yanayoisambaza bidhaa hiyo na hawana namna ya kugharamia hilo linaeleza shirika hilo la msaada.

Kutokana na hali hiyo, takwimu za mwezi Mei za shirika la kimataifa kufuatilia masuala ya njaa zinaashiria kuwa nusu ya watoto walio na umri wa chini ya miaka 5 wana utapia mlo sugu nchini Somalia.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW