1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiCuba

Cuba gizani baada ya umeme kukatika nchi nzima

Sylvia Mwehozi
19 Oktoba 2024

Cuba imekumbwa na tatizo la kukatika kwa umeme nchi nzima baada ya mojawapo ya mitambo mikuu ya kuzalisha umeme kushindwa kufanya kazi na kusababisha gridi ya taifa ya umeme kuzimwa.

Cuba-Havana
Mwanamke akiwa amefanya kazi katika mgahawa wakati wa tatizo la kukatika umemePicha: Norlys Perez/REUTERS

Serikali ya Kikomonisti tayari ilikuwa imezifunga shule na taasisi nyingine na kuwarudisha majumbani wafanyakazi wengi wa serikali katika juhudi za kuokoa umeme.

Wizara ya nishati nchini humo imesema katika taarifa yake kuwa kituo cha kuzalisha umeme cha Antonio Guiteras, ambacho ni kikubwa zaidi na chenye ufanisi mkubwa, kilizima na kusababisha hitilafu kwenye gridi ya taifa na kuwaacha takriban watu milioni 10 bila umeme. Maafisa hawakusema ni nini kimesababisha mtambo huo kuzima.

Kukatika kwa umeme kunaashiria hali mbaya katika kisiwa hicho ambacho maisha yamezidi kuwa magumu, huku wakazi tayari wakikabiliwa nauhaba wa chakula, mafuta, maji na dawa. Rais wa Cuba Miguel Diaz-Canel alisema kupitia mtandao wa X kwamba watafanya kila wawezalo kurejesha umeme.

Madereva wakisubiri kujaza mafuta mjini HavanaPicha: ADALBERTO ROQUE/AFP

Kukatika kwa umeme kulikuwa tayari kumechangia serikali kufuta huduma zote zisizo muhimu za serikali siku ya Ijumaa. Shule pamoja na vyuo vikuu, vimefungwa hadi Jumapili. Shughuli za burudani na kitamaduni pamoja na vilabu vya usiku, pia vimeamriwa kufungwa. 

Takriban biashara zote katika mji mkuu wa Havana zilisimama siku ya Ijumaa. Wakazi wengi waliketi wakitokwa na jasho kwenye milango. Watalii wengi pia wameathirika na adha hiyo.

"Tulienda kwenye mgahawa na hawakuwa na chakula kwa sababu hapakuwa na umeme, sasa pia hatuna mtandao," alisema mtalii kutoka Brazil Carlos Roberto Julio, ambaye aliwasili mjini Havana hivi karibuni.

Soma pia: Marekani yakosolewa na Iran kwa kuunga mkono maandamano ya Cuba

Waziri Mkuu Manuel Marrero alisema siku ya Alhamis kuwa tatizo la kukatika kwa umeme katika wiki kadhaa zilizopita limechangiwa zaidi na dhoruba, kuzorota kwa miundombinu, uhaba wa mafuta na kuongezeka kwa mahitaji. "Uhaba wa mafuta ni sababu kubwa", alisema Marrero katika ujumbe kwa taifa kwa njia ya televisheni.

Maafisa wanasema upepo mkali ulioanza na Kimbunga Milton wiki iliyopita umelemaza uwezo wa kisiwa hicho kusambaza mafuta kutoka katika maboti nje ya nchi hadi kwenye mitambo yake ya kuzalisha umeme.

Wakazi wa Havana wakiwa mitaaniPicha: MARIANA SUAREZ/AFP

Serikali ya Cuba pia inalaumu vikwazo vya kibiashara vilivyowekwa na Marekani, pamoja na vikwazo vipya chini ya Rais wa zamani Donald Trump, kama ambavyo vimechangia upatikanaji wa mafuta na vipuri vya kuendesha mitambo yake inayotumia mafuta.

Soma kwa kina: Manowari zakivita kwenda Havana, Cuba wiki ijayo katika 'uhusiano wa kirafiki'

Wakati mahitaji ya umeme yameongezeka usambazaji wa mafuta umepungua. Muuzaji mkubwa wa mafuta wa Cuba, Venezuela, amepunguza usafirishaji kwenda kisiwa hicho hadi wastani wa mapipa 32,600 kwa siku katika miezi tisa ya kwanza ya mwaka.

Urusi na Mexico, ambazo siku za nyuma zilituma mafuta nchini Cuba, pia zimepunguza sana usafirishaji kwenye kisiwa hicho.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW