1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mamilioni ya Waislamu duniani waadhimisha Eid al-Fitr

2 Mei 2022

Mamilioni ya waislamu kwenye mataifa kadhaa duniani leo wanasherehekea sikukuu ya Eid Al-Fitr baada ya kukamilika kwa nguzo muhimu ya kidini ya kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Pakistan Eid al-Fitr
Picha: AAMIR QURESHI/AFP/Getty Images

Sherehe za mwaka huu zinafanyika chini ya kiwingu cha kupanda kwa bei za vyakula ulimwenguni kulikochochewa na vita vinavyoendelea nchini Ukraine huku maeneo mengine yakiwa bado yanaandamwa na mizozo.

Nchini Indonesia, taifa lenye idadi kubwa ya waislamu duniani, sherehe ya Eid inaadhimishwa leo kwa uhuru mkubwa baada ya kuondolewa kwa vizuizi vya kukabiliana na janga la virusi vya corona vilivyodumu kwa miaka miwili.

Sikukuu ya Eid, moja ya sherehe muhimu katika kalenda ya Waislamu huadhimishwa kwa ibada ya pamoja, dhifa ya chakula, manunuzi ya nguo mpya na waumini kutembeleana.

Sherehe za Eid al-FitrPicha: Emrah Gurel/AP/picture alliance

Uganda nayo yaadhimisha Eid al-Fitr

Jumuiya ya Waislamu nchini Uganda imetoa wito kwa serikali kutafuta ufumbuzi kuhusu suala zima la mfumko wa bei za bidhaa muhimu. Hata hivyo, waislamu kwa jumla wanashukuru kwamba licha ya hali hiyo ngumu wameweza kushiriki mfungo wa mwezi wa Ramadhan kwa amani nakuweza kujikimu mahitaji yao muhimu.

Katika msikiti mkuu wa Mlimani Kibuli ambapo umati wa waumini wa Kiislamu, wake kwa waume wamehudhuria swala ya Idd. Wote wamedhihirisha furaha na bashasha kuweza kutimiza nguzo ya nne ya Kiislamu kwa kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhan kwa siku 30. Furaha hii ni kwamba hata katika hali ngumu ya mfumko wa bei za bidhaa muhimu za matumizi ya nyumbani  hususan vyakula, wamejaaliwa kufika siku ya leo na kufanya kila jitihada kuona kwamba familia zao zinasherehekea ipasavyo.

Kero ya mfumko wa bei za bidhaa ndiyo imetawala ujumbe wa viongozi wa kidini siku hii ya Idd Ul Fitri katika misikiti yote mikuu ikiwemo ule wa Gaddafi. Mufti wa Uganda Sheikh Shaban Ramadhan Mubajje.

Mwito mwingine kuhusiana na uchumi wa nchi ambao viongozi wa kidini wametoa kwa serikiali ni kwamba ibadili msimamo wake kuhusu biashara ya kahawa ambapo tajiri mmoja mwanamke raia wa Italia amesaini mkataba wa miaka kumi kununua kahawa yote inayozalishwa Uganda. Kwingineko vijana wa kike wameibuka washindi katika mashindano ya kusoma Qur'an. Hii imekuwa miongoni mwa tamasha ambazo zinashuhudiwa hii leo katika sherehe za Iddi. Zeitun Uthman ni mmoja kati ya washindi hao.

Kwa jumla familia zimeshuhudiwa zikiwa katika pilkapilka za mapishi na kuwakaribisha majirani, hii pia ikiwa siku ya mapummziko Uganda. Ikumbukwe kuwa hii ndiyo iddi ya kwanza katika miaka miwili kwa waislamu kujumuiya pamoja tangu mwaka 2019 kabla ya mripuko wa ugonjwa wa COVID-19.

 

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW