1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mdahalo wa Televisheni kati ya Biden na Trump

27 Juni 2024

Je nani atafanikiwa kuwashawishi wapiga kura katika mdahalo wa Tv kati ya wagombea urais Joe Biden na Donald Trump?

KOMBO Trump Biden
Picha: ABACA/IMAGO;AP Photo/picture alliance

Nchini Marekani macho yote yataelekezwa leo Alhamisi kwenye televisheni kutazama mpambano wa mdahalo muhimu kati ya Rais Joe Biden na Donald Trump, wagombea wawili katika kinyang'anyiro cha uchaguzi wa rais.

Mdahalo huu ni muhimu kwa wagombea wote wawili katika wakati huu wakipambana kuwashawishi wapiga kura na hasa wale ambao hadi sasa hawajaamuwa nani wanataka kumpa kura zao.

Kituo cha kupiga kura-South CarolinaPicha: Allison Joyce/AFP/Getty Images

Mamilioni ya Wamarekani wanatarajiwa kufuatilia mdahalo huu wa leo Alhamisi uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu kubwa na ambao ni kipenga cha kuanza msimu wa kampeini moto moto katika kipindi hiki cha majira ya joto katika taifa hilo ambalo kwa kiasi kikubwa liko katika haki ya mashaka na ambao bado haijasahau vurugu na mparaganyiko ulioshuhudiwa katika uchaguzi wa mwaka 2020.

Huku kukiwa na midahalo miwili tu katika uchaguzi wa mara hii na kura za maoni zikionesha ushindani ni mkali mno kwa wagombea hawa wawili, mdahalo wa leo unaofanyika katika makao makuu ya kituo cha televisheni cha Marekani cha CNN mjini Atlanta katika jimbo la Georgia, unabeba umuhimu mkubwa sana.

Kwa wapiga kura wengi kuchagua kati ya rais anayetetea nafasi yake Joe Biden na mpinzani wake wa muda mrefu Donald Trump ambaye kimsingi ni mshtakiwa wa uhalifu, sio kitu cha kinachowavutia,na kwa maana hiyo wagombea hawa wawili wazee wote wanahitaji kuonesha namna wanavyoweza kuwashawishi wapiga kura kwenye mdahala huu wa ana kwa ana.

Mgombea urais Donald TrumpPicha: TIMOTHY A. CLARY/AFP

Kwa Trump kibarua kikubwa kinachomkabili itakuwa ni kujizuia kuonesha hasira zake za waziwazi kuelekea kwa Biden kuepusha kilichoshuhudiwa katika mdahalo wao wa mwanzo miaka minne iliyopita.

Trump ameshakiambia kituo cha NewsMax kwamba amejiandaa katika kipindi cha maisha yake yote na kwahivyo anaamini atafanya vizuri.

Ama kwa rais Biden mwenye umri wa miaka 81 kikubwa atakachohangaika kukiepuka ni kufanya kosa lolote la kuropoka yasiyohusu,ambayo yanaweza kuwekea mstari wasiwasi uliopo kuhusu umri wake.

Atalazimika kuwa makini mno kubakia kwenye mstari,kutowa kwa ufasaha ujumbe wake muhimu kwenye kampeini yake ambao ni kuwaonesha wapiga kura kwamba Donald Trump ni kitisho kwa Demokrasia ya taifa hilo.

Rais Joe Biden- mgombe wa DemocratsPicha: Stephanie Scarbrough/AP Photo/picture alliance

Mara hii mpambano huu utafanyika studio bila ya watazamaji, hali ambayo itawanyima wagombea hao shangwe ya moja kwa moja kutoka kwa wafuasi wao, na utakwenda kwa dakika 90.

Ripoti zinaonesha kwamba Wamarekani waliowengi wanatarajia Trump atashinda mdahalo huu dhidi ya Biden.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW