Mamlaka ya Iran imeongeza msako dhidi ya wanaharakati
21 Agosti 2023Human Rights Watch imesema kwenye ripoti yake iliyotolewa leo kwamba mamlaka katika Jamhuri hiyo ya Kiislamu ziliyadhibiti kikatili maandamano ya kuipinga serikali yaliyozuka baada ya kifo cha Mahsa Amini, msichana wa Kikurdi aliyekuwa na umri wa miaka 22, aliyekufa akiwa chini ya ulinzi wa polisi mnamo Septemba 16, 2022.
Soma pia:Umoja wa Mataifa walaani ukandamizaji wa Iran
Shirika hilo linadai kuwa mamia ya watu waliuawa na maelfu ya waandamanaji walikamatwa.
Mnamo Agosti 16, kundi linalopigania haki za wanawake nchini Iran, Bidarzani, liiliripoti kwamba vikosi vya usalama vilifanya msako majumbani na kuwakamata watu 12, wakiwemo watetezi 11 wa haki za wanawake.
Aidha Bidarzani imeripoti kwamba Ofisi ya Mwendesha Mashtaka nchini Iran imekataa kutoa taarifa kwa familia kuhusu mashtaka dhidi ya waliokamatwa.
Soma pia: Iran yawanyonga watatu kwa mauaji ya polisi
Agosti 17, shirika la habari la Tasnim, ambalo liko karibu na shirika la kijasusi la Iran liliripoti kwamba Ofisi ya Ujasusi ya Mkoa wa Gilan ilitoa taarifa ikisema kuwa imeukamata mtandao wa watu 12 kwa madai ya "kupanga kuvuruga usalama."
Makosa yasiyoeleweka
Kwa mujibu wa shirika la Human Rights Watch, vyombo vya kijasusi na mahakama mara kwa mara huwashutumu wanaharakati kwa matukio yasiyoeleweka ya usalama katika kesi ambazo zina mapungufu makubwa katika viwango vya kimataifa.
Shirika hilo linasema katika wiki iliyopita, mamlaka zimewaita na kuwakamata wanaharakati wengine, miongoni mwao ni Mahsa Basir Tavana, dada yake Mehran Basir Tavana, ambaye aliuawa wakati wa maandamano ya kupinga serikali ya 2022.
Shirika hilo pia iliripoti kwamba mnamo Agosti 16, maafisa wa ujasusi walimkamata mwanablogu Elaheh Asgari, na kumhamishia kwenye gereza la Evin baada ya kwenda kwenye ofisi ya pasipoti kujaribu kupata hati yake ya kusafiria aliyokuwa amepokonywa.
Msako wa kidini
Katika wiki za hivi karibuni, mamlaka pia zimeongeza msako dhidi ya jamii ya wachache wa dini ya Bahai. Jumuiya ya Kimataifa ya Bahai (BIC), imesema waumini 11 wa jamii ya hiyo wamekamatwa. Miongoni mwao ni Jamaluddin Khanjani, kiongozi wa zamani wa jamii ya Baha'i mwenye umri wa miaka 90 ambaye alikuwa ametumikia kifungo cha miaka 10 gerezani, pamoja na binti yake, Maria Khanjani.
Soma pia: Iran yatoa hukumu ya kifo kwa waandamanaji
Human Rights Watch imesema kuwa serikali ya Iran inafanya kila iwezalo kuzuia matukio ya kuandaa ibada za kumbukumbu zinazofanywa na familia za waandamanaji waliouawa mwaka 2022.
Tazama:
Chanzo/ https://www.hrw.org/news/2023/08/19/iran-mass-arrests-womens-rights-defenders