1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Man City, Inter Milan zatinga robo fainali, Champions League

15 Machi 2023

Timu nne zimekuwa zikiwania nafasi ya kufuzu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya Champions League.

Fußball | Champions League | Manchester City - RB Leipzig | Erling Braut Haaland
Picha: Dave Thompson/AP Photo/picture alliance

Timu ya RB Leipzig ya Ujerumani wanaotiwa makali na kocha Marco Rose walipewa kichapo cha adabu cha mabao 7-0 na timu ya Manchester City ya England katika uwanja wa Etihad. Kikosi cha Pep Guardiola kinatinga robo fainali kwa ushindi wa jumla ya mabao 8-1.

Katika mechi hiyo, mchezaji Erling Haaland alifunga mabao matano akianza na mkwaju wa penati na kisha kuongeza mabao mengine manne na hivyo kuwa mchezaji wa tatu katika historia ya Ligi ya Mabingwa kufunga mabao matano katika mchezo mmoja. Rekodi hiyo ilikuwa inashikiliwa na Lionnel Messi alipokuwa Barcelona pamoja na Luiz Adriano wa Shakhtar Donetsk.

Ulikuwa ni usiku wa kuvunja rekodi kwa Haaland mwenye umri wa miaka 22, ambaye alikua mfungaji bora wa Manchester City katika msimu mmoja alipotimiza mabao 39 na kumpiku Tommy Johnson aliekuwa na mabao 38 na aliyeichezea Manchester City miaka ya 1928-29.

Erling Haaland: (wa kwanza kulia) akisherehekea bao lake la tatu dhidi ya RB Leipzig, 14.03.2023 katika uwanja wa EtihadPicha: Dave Thompson/AP/picture alliance

Haaland anakuwa pia mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kufikisha mabao 30 katika michuano ya Champions League, ambapo sasa ana jumla ya mabao 33 katika jumla ya mechi 25 alizoshiriki katika michuano hii ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya.

Mchezaji raia wa Ubelgiji Kevin De Bruyne aliyerejea kikosini baada ya jeraha alihusika katika mabao sita katika usiku utakaosalia kuwa kumbukumbu katika uwanja wa huo wa Etihad.

FC Porto wayaaga mashindano licha ya mchezo wa kuvutia

Katika mechi nyingine, Inter Milan wamefanikiwa kufuzu baada ya kutoka sare ya kutofungana na FC Porto ambayo ilikosa magoli kadhaa katika mechi hiyo. Ikumbukwe kuwa katika mechi ya awali Inter Milan walipata ushindi mwembamba wa bao 1-0, lililotiwa nyavuni na mchezaji Romelu Lukaku.

Inter Milan ambao ni washindi mara tatu wa Champions League walikuwa hajafuzu hadi nane bora tangu mwaka 2011 na tangu mwaka 2006 ndio kwa mara nyingine tena wamefuzu robo fainali.

Romelu Lukaku wa Inter Milan akishangilia na Christian Eriksen baada ya kufunga bao lake katika mechi na Lazio,Februari 14, 2021Picha: Marco Luzzani/Getty Images

Inter ilijiweka katika mazingira magumu kwenye Uwanja wa Estadio do Dragao huku Porto wakiwa na matokeo bora zaidi ya mchezo lakini walishambulia mara chache lango la kipa wa Inter Milan Andre Onana na hivyo kushindwa kufuzu. Katika dakika za lala salama, Porto walipata nafasi nzuri za kupata ushindi bila mafanikio.

Soma pia: Liverpool, Madrid kuumana Ligi ya Mabingwa

Manchester City na Inter Milan wanaungana na Bayern Munich, Chelsea, Benfica na AC Milan ambazo zimefuzu wiki iliyopita. Hatua ya 16 bora itakamilika leo Jumatano wakati mabingwa watetezi Real Madrid watakapokutana na Liverpool. Katika mechi ya awali Real Madrid walipara ushindi wa mabao matano kwa mawili dhidi ya Liverpool. Napoli itachuana na Eintracht Frankfurt. Droo ya robo fainali itafanyika siku ya Ijumaa.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW