1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MichezoUingereza

Manchester City yachupa kileleni mwa Ligi Kuu ya Premia

1 Mei 2023

Manchester City imechupa kileleni mwa Ligi Kuu ya Premia kwa mara ya kwanza baada ya kupata ushindi mwembamba wa 2-1 dhidi ya Fulham.

Manchester City - FC Arsenal
Mshambuliaji wa Manchester City Erling HaalandPicha: Dave Thompson/AP/dpa/picture alliance

Hio ni mara ya kwanza kwa vijana wa Pep Guardiola kushikilia nafasi hiyo tangu Februari 17. Kwa ujumla Arsenal imekuwa kileleni kwa siku 247.

Mabao ya mshambuliaji matata Erling Haaland na Julian Alvarez yameweka hai matumaini ya Manchester City kutetea ubingwa kuelekea mechi sita za mwisho.

Ushindi huo umeiweka Manchester City kileleni mwa jedwali ikiwa na alama 76, alama moja mbele ya Arsenal yenye alama 75.

Soma pia: Guardiola: Arsenal ya msimu huu ni kitisho

"Sikuwa na shaka yoyote kuhusu mchezo wa leo.Mechi ilikuwa ngumu mno hadi dakika ya mwisho, na hatukurarajia chochote tofauti," Guardiola ameeleza.

Hii leo usiku, vibonde Leicester watateremka uwanjani King Power kupambana na Everton kabla ya Arsenal kumaliza udhia na Chelsea kesho Jumanne uwanjani Emirates.

Kuelekea dabi hiyo ya London, kocha wa Chelsea Frank Lampard amesema, "Matokeo yanaweza kwenda vyovyote vile. Nadhani Arsenal bado ina uwezo wa kushinda Ligi, maana wamekuwa na mchezo mzuri msimu huu. Ndio, wameteleza kidogo na huenda hilo likawapa msukumo. Lakini kama tutafanya mambo kuwa magumu kwao, mchezo huenda ukawa tofauti."