Manchester United yatinga nusu fainali Europa League
11 Agosti 2020Mechi zote za robo fainali zilichezwa nchini Ujerumani kama sehemu ya kumalizia hatua ya mwisho ya mashindano, ambayo yalisimamishwa kwa kipindi cha miezi mitano kutokana na janga la mlipuko wa virusi vya Corona. Manchester United walizawadiwa mkwaju wa penalti mapema, lakini penalti hiyo ilifutwa kupitia teknolojia ya uamuzi wa video, VAR, iliyomuonyesha mchezaji Harry Maguire kuwa alikuwa amejenga kibanda.
Mshambuliaji chipukizi Mason Greewood alidhani alikuwa amefunga bao dakika za mwisho za kipindi cha kwanza ambacho hakikuwa kizuri kimchezo, lakini goli likaondolewa katika kumbukumbu kwa mara nyingine kutokana na kuwa alikuwa ameotea.
Copenhagen walikuwa wakichanganya kwa kuonyesha mvuto na nidhamu na kikosi cha kocha Ole Gunnar Solskjaer, hawakuwa katika makali yao kama walivyomaliza msimu wa ligi kuu ya England.
Greenwood aligonga mchuma wa lango mapema katika kipindi cha pili na Rashford akautia mpira kimyani lakini kwa mara nyingine alikuwa ameotea. Bruno Fernandes kisha akagongesha tena nguzo ya goli, mara ya nane Mashetani Wekundu kugonga besela katika ligi ya Ulaya msimu huu, wakati United ilipokuwa ikikaza skurubu.
Kiungo mchezeshaji mwenye ujuzi wa Copenhagen Rasmus Falk alitishia upande wa Man United, wakati mlinda mlango hodari Karl-Johan Johnsson akimzuia Martial Anthony kukata kamba.
Mwishowe mafanikio yalikuja katika muda wa ziada, wakati Andreas Bjelland alipoadhibiwa vikali kufuatia kumtendea madhambi Martial katika eneo la hatari. Bruno alikwamisha penalti yake ya saba katika msimu bila kikwazo chochote na kuipeleka Machester United mbele katika mashindano hayo ikisubiria kukutana na uso kwa uso na Wolves au Sevilla katika hatua ya nusu fainali.
"Tulistahili kushinda usiku huu. Mlindalango wao alikuwa bora, alikuwa hatabiriki,” alisema kocha wa Mashetani Wekundu, Solskjaer.
Inter wawapiga kumbo Leverkusen
Kwa upande wao Inter Milan walianza kwa nguvu katika usiku uliouwa na joto mjini Dusseldorf na ikapata bao la kwanza kupitia Nicolo Barella kunako dakika ya 15.
Lukaku alisababisha sekeseke katika eneo la hatari na kuachilia shuti kali ambalo lilizuiliwa, lakini mchezaji mwenzake alimalizia kwa kukwamisha mpira kimiani na kuiweka kifua mbele timu yake. Mbeligiji huyo aliingia katika orodha ya wafungaji magoli dakika sita baadaye na kombora la kijanja huku akianguka baada ya kumzidi kete Edmond Tapsoba.
Lukaku aliweka rekodi mpya ya ufungaji katika mechi tisa mfululizo ikiwa ni pamoja na michezo mitano kwa Everton mnamo msimu wa mwaka 2014 na 2015, na kufikisha jumla ya magoli 31 katika mashindano yote.
Kai Havertz aliifungia Leverkusen bao maridadi baada ya kupokea pasi kutoka kwa Kelvin Volland na kuyaweka matumai ya timu yake kusonga mbele.
Inter walizawadiwa penalti baada ya Daley Sinkgraven wa Leverkusen kuunawa mpira katika eneo la adhabu, lakini mitambo ya VAR ilionyesha Sinkgraven aliuzuia krosi kwa bega lake.
Robo fainali nyingine itapigwa Jumanne (11.08.2020) kabla ya mechi za nusu fainali kuanza siku ya Jumapili.